62% ya Wazayuni wanataka vita dhidi ya Ghaza vikomeshwe
Jul 27, 2024 08:57 UTC
Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa na chaneli ya 12 televisheni ya Israel yanaonyesha kuwa asilimia 62 ya Wazayuni wanataka kukomeshwa vita dhidi ya Ukanda wa Ghaza.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni, Wazayuni wengi wanaamini kuwa, kuwarejesha mateka wa Kizayuni ni muhimu zaidi kuliko kuendeleza vita dhidi ya Ghaza, ili kwa dhana yao, upatikane ushindi.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa maoni ni asilimia 29 tu ya Wazayuni wanaamini kuwa kuendelezwa vita hivyo ni muhimu zaidi kuliko kuachiliwa huru mateka wa Israel.
Sehemu nyingine ya ripoti ya uchunguzi huo wa maoni imeeleza kuwa, asilimia 51 ya Wazayuni wanaamini kwamba kutokana na maslahi na mazingatio ya kisiasa ya waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benyamin Netanyahu, makubaliano ya kubadilishana mateka na Muqawama wa Palestina hayatatekelezwa.
Tovuti ya Times of Israel nayo pia iliripoti siku ya Jumamosi kuwa, mwanajeshi mmoja wa Israel alijiua baada ya kupewa amri ya kurejea Ukanda wa Ghaza kwa ajili ya kuhudumu jeshini.
Katikati ya mwezi uliopita wa Machi, jeshi la utawala wa Kizayuni lilikiri kwamba askari wa utawala huo wamekabiliwa na tatizo kubwa zaidi la afya ya akili.
Wakati huo huo jeshi la Kizayuni linaendelea kukataa kutangaza habari za kushindwa kwenye mapigano na kuweka hadharani takwimu za idadi ya wanajeshi wake waliouawa katika vita vya Ghaza.
Baada ya kupita takriban miezi 10 tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha uvamizi usio na tija dhidi ya Ukanda wa Ghaza, utawala huo unazidi kuzama kwenye kinmasi cha migogoro yake ya ndani na nje na haujaweza hadi sasa kufikia malengo yake, ambayo ni kuuangamiza Muqawama wa Palestina na kuwakomboa mateka wa Kizayuni wanaoshikiliwa katika ukanda huo.../
Tags