Jul 29, 2024 02:33 UTC
  • Syria: Israel yenyewe imeshambulia Majdal Shams ili kupata kisingizio cha kupanua vita

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imesema, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umefanya shambulio katika eneo la Majdal Shams lililoko kwenye Miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu ili kuhalalisha lengo lake la kutaka kupanua wigo wa vita na uvamizi wake wa kijeshi katika eneo.

Wizara hiyo imeeleza katika taarifa yake kwamba utawala ghasibu wa Israel umefanya jinai ya kutisha katika mji wa Majdal Shams na kisha kuubebesha dhima ya jinai hiyo Muqawama wa Kitaifa wa Lebanon.
 
Taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imefafanua kuwa jinai hiyo ya utawala wa Kizayuni iko katika mpango unaofuatiliwa na utawala huo ghasibu wa kuifanya hali ya mambo iwe mbaya zaidi na kupanua wigo wake wa uvamizi katika eneo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wananchi wa Syria wanaoishi katika Miinuko ya Golan wamekuwa, wangali, na wataendelea kuwa sehemu muhimu ya Muqawama dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni na sera zake za kichokozi.

 
Eneo la Majdal Shams lililoko kwenye Miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na Israel lilishambuliwa kwa kombora siku Jumamosi jioni. Shambulio hilo liliua watu 12 na kujeruhi wengine kadhaa.
 
Kufuatia shambulio hilo, vyombo vya habari na maafisa wa utawala wa Kizayuni waliielekezea kidole cha tuhuma Hizbullah kuwa ndio iliyohusika na hujuma hiyo, lakini harakati hiyo wa Muqawama wa Lebanon ilieleza bayana katika taarifa kwamba haihusiki kwa namna yoyote na shambulio la Majdal Shams.
 
Baadhi ya duru za habari zimefichua kuwa chanzo cha tukio hilo la Majdal Shams huko Golan inayokaliwa kwa mabavu ni kombora la kutungulia ndege la utawala wa Kizayuni ambalo lilipiga uwanja wa mpira wa eneo hilo.../

 

 

Tags