HAMAS: Badala ya mazungumzo mapya, Wazayuni walazimishwe kutekeleza usitishaji vita
Aug 13, 2024 05:40 UTC
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema utawala ghasibu wa Kizayuni umethibitisha kuwa hautaki kufikia makubaliano; na kwa sababu hiyo, harakati hiyo imewataka wapatanishi wa Misri na Qatar wawalazimishe Wazayuni watekeleze pendekezo la hivi karibuni la usitishaji vita badala ya kutaka yaanzishwe mazungumzo mengine mapya.
Wakati utawala dhalimu wa Kizayuni unashadidisha mashambulio yake ya kinyama dhidi ya Ukanda wa Ghaza huku zikitangazwa habari za kupendekezwa yafanyike mazungumzo mapya ya kujadili usitishaji vita na kubadilishana mateka, harakati ya Hamas imetoa taarifa ikiwataka wasuluhishi hao watekeleze mpango waliokuwa wameuwasilisha kwa harakati hiyo na kuulazimisha utawala wa Kizayuni uutekeleze mpango huo.
Hamas imesema katika taarifa hiyo: "tangu zilipoanza hujuma na uvamizi wa adui, tulisisitiza juu ya kufanikiwa juhudi za wapatanishi wa Misri na Qatar kufikia makubaliano ya usitishaji vita na kuhitimisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi wa Palestina, na tuliunga mkono juhudi zote za kukomesha uchokozi".
Harakati hiyo ya Muqawama ya Palestina imeashiria taarifa ya pande tatu ambayo ilitolewa hivi karibuni na Misri, Qatar na Marekani kuhusu mazungumzo ya kusitisha mapigano Ghaza, na kusisitiza kwa kusema: "sisi tumeshafanya duru nyingi za mazungumzo na tumelegeza msimamo na kuonyesha nia njema kila ilipohitajika kufanya hivyo, ili kufikia malengo na maslahi ya taifa letu, kuepusha kumwagwa damu za watu wetu na kukomesha mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi wetu".
Taarifa hiyo ya Hamas imeendeleza kueleza: "kuhusiana na suala hili, mnamo Mei 6, 2024 harakati yetu ilikubali pendekezo la wapatanishi la kusitisha mapigano na kukaribisha tangazo la Rais wa Marekani Joe Biden mnamo Mei 31 pamoja na Azimio nambari 2735 la Baraza la Usalama kuhusiana na suala hilo. Lakini adui alikataa mipango hiyo na kuendeleza jinai dhidi ya taifa letu".
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hata baada ya kutangazwa taarifa ya hivi karibuni ya pande tatu kuhusu mazungumzo ya kusitisha mapigano, adui Mzayuni alitenda jinai mbaya kwa kuwaua wakimbizi wa Skuli ya al-Tabaeen katika kitongoji cha al-Daraj.
Kabla ya hapo, nchi tatu za Misri, Qatar na Marekani zilitoa tamko la pamoja na kusisitiza kuwa makubaliano jumla yapo mezani na ni ufafanuzi wa utekelezaji wake tu ndio unaopasa kukubaliwa na pande mbili husika.../