Netanyahu na uafriti wake usio na kikomo wa kukwamisha mapatano katika mazungumzo ya kusimamisha vita
Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel anaendelea kukwamisha mapatano katika mazungumzo ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Ghaza.

Netanyahu na baadhi ya mawaziri wake ndio kizuizi kikubwa zaidi kinachokwamisha kufikiwa mwafaka katika mazungumzo ya kusitisha mapigano, kwa sababu kila inapotangazwa habari ya kutia matumaini kuhusiana na mazungumzo hayo, huzua uafriti mpya wa ukwamishaji. Katika uafriti wake wa karibuni zaidi, siku ya Jumatatu Netanyahu alidai kuwa harakati ya Hamas inapata silaha kupitia Misri na Ukanda wa Philadelphia.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imetangaza katika taarifa kwamba: kwa kauli yake hiyo, na kwa kulipenyeza jina la Misri kwenye madai yake, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni anataka kukwamisha tena juhudi za kufikia mapatano na kuwababaisha Waisraeli kuhusiana na suala hilo. Siku ya Jumanne, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq ilitoa taarifa ya kulaani madai ya waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni kwamba silaha zinaingizwa Ghaza kutokea Misri. Taarifa hiyo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq ilieleza bayana kuwa: Baghdad inalaani vikali matamshi ya utawala ghasibu wa Kizayuni ya kukwamisha juhudi za kusitisha vita huko Ghaza na inatangaza mshikamano na Misri dhidi ya madai hayo ya uwongo yaliyotolewa kuhusu mhimili wa Philadelphia.

Uafriti unaofanywa na Netanyahu na baraza lake la mawaziri wa kukwamisha kufikiwa mwafaka katika mazungumzo unatokana na sababu kadhaa. Sababu ya kwanza ni kwamba, hakuna makubaliano ya pamoja ndani ya baraza lake la mawaziri juu ya suala la kusitisha vita katika Ukanda wa Ghaza; na kuna baadhi ya mawaziri wenye misimamo mikali ambao wamefika hadi hata kumuonya Netanyahu kuwa watachukua hatua ya kujiuzulu katika serikali yake endapo vita vitasitishwa huko Ghaza na hivyo kuandaa mazingira ya kusambaratika serikali hiyo. Sababu ya pili ni kuwa, Netanyahu anafahamu kwamba kumalizika vita huko Ghaza kunaweza kuchochea juhudi za mrengo wa upinzani za kutamatisha maisha yake ya kisiasa, kwa sababu miezi 11 ya vita dhidi ya Ghaza haijawezesha kukombolewa mateka na kurejeshwa heshima na itibari ya taasisi za kiintelijensia na kijeshi za utawala huo. Kuhitimishwa vita vya Ghaza na kuondoka kikamilifu majeshi ya Kizayuni katika eneo hilo ni jambo linalomtia hofu na kiwewe Netanyahu kwa sababu analichukulia kama ithibati kamili ya kushindwa vibaya sana katika njama yake dhidi ya Muqawama, Ghaza na Palestina kwa ujumla.../