Sep 09, 2024 02:15 UTC
  • Mazungumzo ya Araghchi na mwenzake wa Yemen kuhusu sisitizo la kuendelea kuwaunga mkono wananchi wa Palestina

Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo ya simu na Jamal Amer, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen ambapo pande mbili zimesisitiza juu ya udharura wa kuendelea kuwaunga mkono wananchi wa Palestina.

Abbas Araghchi, amesema katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Yemen kwamba uhusiano wa Iran na Yemen na kuendelezwa mashauriano ya pande mbili kwa shabaha ya kuchangia usalama wa eneo kuna umuhimu mkubwa sana. Katika mazungumzo hayo ya simu, Araghchi ameongeza kuwa wakati ambapo nchi nyingi zimetosheka kwa kutangaza tu misimamo dhidi ya utawala wa Kizayuni, serikali na wananchi wa Yemen wamekuwa wakikabiliana kivitendo na ukandamizaji unaofanywa na utawala huo katili dhidi ya wananchi wa Palestina.

Jamal Amer, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen pia amesema katika mazungumzo hayo ya simu na mwenzake wa Iran kwamba msimamo wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen katika kuliunga mkono taifa madhulumu la Palestina hautabadilika hata kidogo na kueleza matumaini yake kuhusu kuimarishwa ushirikiano wa nchi mbili katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kisiasa.

Mazungumzo ya simu ya Abbas Araghchi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen 

Tangu kuanza Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa ya makundi ya muqawama ya Palestina  tarehe 7 Oktoba mwaka jana dhidi ya utawala katili wa Kizayuni, wanaharakati wa Muqawama wa Iraq, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon Hizbullah pamoja na Harakati ya Ansarullah ya Yemen zimekuwa zikiwatetea kivitendo watu wa Palestina ambapo zimelenga vituo vya kijeshi na kijasusi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel huko Palestina. Mashambulizi hayo ya vikosi vya muqawama na jeshi la Yemen dhidi ya Wazayuni yamekuwa na taathira kubwa katika matukio ya eneo, ambapo viongozi wa utawala huo ghasibu daima wamekuwa wakikiri kutokuwa na uwezo wa kukabiliana nayo.

Jeshi la Wanamaji la Yemen pia limeingilia kati kuwaunga mkono wananchi wa Palestina ambapo limezuia meli za utawala wa Kizayuni na za nchi za Magharibi zinazouunga mkono na hasa za Marekani kupita katika Bahari Nyekundu kuelekea au kutoka katika bandari za utawala huo katika ardhi unazokaliwa kwa mabavu. Viongozi wa jeshi la Yemen pia wanasisitiza mara kwa mara kuwa wataendelea kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na wala hawatawaacha wateseke peke yao.

Wayamen kuendelea kuwaunga mkono Wapalestina

Mohammed Nasser Al-Atafi, Waziri wa Ulinzi wa Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemen, amesisitiza kuwa majibu makali ya Yemen kwa utawala wa Kinazi na Kizayuni wa Israel bila shaka yatatekelezwa bila wasiwasi wowote na kuwa wazimu wa Wazayuni utakabiliwa na machungu ambayo tayari wameshayaonja baharini. Mohammed Nasser Al-Atafi ameongeza kuwa nafasi ya Yemen katika mhimili wa Jihad na muqawama ni jambo la msingi katika kutetea umma na matukufu yake, thamani na ardhi zake na usalama wa taifa la Yemen.

Mazungumzo ya simu ya Araghchi na mwenzake wa Yemen ni ishara nyingine ya ushirikiano wa kieneo na azma ya Iran ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kukabiliana na utawala wa Kizayuni na muungaji mkono wake mkuu, Marekani. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa na nafasi muhimu katika kuvisaidia vikosi vya muqawama katika eneo hili, ambapo mashauriano ya karibuni ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na mwenzake wa Yemen yanahesabiwa kuwa muendelezo wa diplomasia ya Tehran kwa ajili ya kuimarisha mhimili wa muqawama.

Mchakato wa matukio ya eneo baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa umeongeza mshikamano na ushirikiano wa makundi ya muqawama katika kuwaunga mkono wananchi wa Palestina, ushirikiano wa kistratijia ambao umeongeza mashinikizo dhidi ya utawala wa Kizayuni. Jeshi na wanamuqawama wa Yemen wamekuwa na nafasi kubwa katika matukio ya vita vya  Gaza, ambapo wamekuwa wakishirikiana na makundi ya muqawama ya Palestina kwa ajili ya kuushinikiza zaidi utawala wa Kizayuni, kwa namna ambayo watawala wa Kizayuni wenyewe hatimaye wamelazimika kukiri kubanwa na mashinikizo hayo.