Jumamosi, Februari 13, 2016
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i1165-jumamosi_februari_13_2016
Leo ni Jumamosi tarehe 4 Mfunguo Nane Jamadi al-Awwal 1437 Hijria sawa na tarehe 13 Februari mwaka 2016 Miladia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 13, 2016 04:51 UTC
  • Jumamosi, Februari 13, 2016

Leo ni Jumamosi tarehe 4 Mfunguo Nane Jamadi al-Awwal 1437 Hijria sawa na tarehe 13 Februari mwaka 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 882 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alizaliwa huko nchini Iraq Ibn Athir Jazari mwanahistoria na mwanafasihi mahiri wa Kiislamu. Ibn Athir alisoma mjini Mosul, Sham na Baghdad kwa maulama watajika kama Khatib Tusi. Alikuwa na mapenzi makubwa na kutwalii na kufanya uhakiki kuhusiana na historia na ni kutokana na sababu hiyo athari zake nyingi zilizoko hii leo zinahusiana na historia. Kitabu mashuhuri zaidi cha Ibn Athir ni kile kinachojulikana kwa jina la "al-Kamil Fi Taarikh." Msomi na mwanahistoria huyo wa Kiislamu alifariki dunia mwaka 630 Hijria katika mji wa Mosul huko Iraq. ***
Katika siku kama ya leo miaka 327 iliyopita tangazo lililojulikana kama Tangazo la Sheria lilisomwa katika sherehe za kumvika taji Mfalme William wa Tatu na Malkia Marry wa Pili wa Uingereza na kuanzia hapo mfumo wa utawala wa nchi hiyo ukabadilika na kuwa utawala wa kifalme wa kikatiba. Kwa mujibu wa tangazo hilo, madaraka ya Mfalme wa Uingereza yalipunguzwa na kukabidhiwa bunge la nchi hiyo. ***
Miaka 28 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Ayatullah Sheikh Salman Khaqani. Alizaliwa mwaka 1293 Hijria Shamsia katika moja ya miji ya kusini mwa Iraq ya leo. Baada ya kupitisha kipindi cha utoto, akiwa na umri wa miaka 13 alihajiri na kuelekea Najaf al-Ashraf kwa ajili ya kusoma masomo ya dini. Akiendelea na masomo yake, Sheikh Salman Khaqani hakuacha kujihusisha na harakati za kijamii, kiasiasa na kifasihi. Akiwa na umri wa miaka 43 na baada ya kufariki dunia baba yake aliyekuwa mmoja wa maulama wa Khorramshahr hapa Iran aliuchagua mji huo kuwa makazi yake. Katika kipindi cha miongo mitatu ya kuishi kwake mjini Khorramshahr, mwanazuoni huyo aliondokea kuwa chimbuko la uongofu wa watu na kufanikiwa kutoa huduma zenye thamani kubwa. Baada ya kuanza vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa Baath wa Iraq, nyumba ya alimu huyo ilikuwa kimbilio la watu.