Hizbullah yaapa kuendelea kuwatetea watu wa Gaza, yasema ukatili wa Israel unaimarisha azma yake ya kupambana na utawala huo
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imeapa kuendeleza mashambulizi yake dhidi ya utawala haramu wa Israel kwa ajili ya kuwatetea watu wa Ukanda wa Gaza, ambao wanaendelea kuuawa kikaktili katika mauaji ya kimbari ya Israel, ikisisitiza kwamba ukatili wa hivi karibuni wa utawala huo ulioua watu kadhaa nchini Lebanon utaimarisha azma yake ya kuendeleza njia ya mapambano na muqawama.
"Tuna uhakika kabisa wa kupata ushindi," imesema taarifa iliyotolewa leo Jumatano ya harakati hiyo.
Taarufa hii ya Hizbullah imetolewa baada ya milipuko iliyotokea kwa wakati mmoja kote Lebanon siku ya jana Jumanne.
Kulingana na kituo cha habari cha Sky News Arabia, Shirika la Ujasusi la Israel Mossad lilitega viripuzi kwenye vifaa vya 'pager' vilivyoripuka jana Jumanne nchini Lebanon, na kuua watu tisa na kujeruhi karibu wengine 2,750, wakiwemo 200 ambao hali zao ni mahututi.
Waliouawa ni pamoja na wanachama wa harakati hiyo la muqawama pamoja na raia wa kawaida.
Hapo awali, Hizbullah ilisema kwamba, baada ya kuchunguza ukweli wote na taarifa zilizopo kuhusu mashambulizi hayo, inautambua utawala wa Israel kuwa "unawajibika kikamilifu kwa jinai hiyo."
Hizbullah imesema "Muqawama wa Kiislamu nchini Lebanon utaendeleza operesheni zake zilizobarikiwa za kuunga mkono Gaza, watu wake, na mapambano ya ukombozi wa Palestina."
"Operesheni hizo pia zitafanyika kutetea Lebanon, watu wake, na uhuru wake," imeongeza taarifa hiyo.
Hizbullah imekuwa ikifanya mashambulizi karibu ya kila siku dhidi ya Israel ikiwa ni kuunga mkono na kuwatetea watu wa Ukanda wa Gaza na mashambulizi makali ya Israel ambayo yamekuwa yakilenga ardhi ya Lebanon tangu kuanzishwa kwa vita mauaji ya kimbari katika ardhi ya Palestina.