Erdogan: Tunasubiri jibu la Rais Assad kwa ombi la kurejesha uhusiano
-
Recep Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki amesema kuhusu mchakato wa kurejesha uhusiano kati ya Uturuki na Syria kwamba, tumesisitiza nia yetu ya kukutana na Rais Bashar al-Assad ili kuanzisha tena uhusiano wa uhusiano kati ya Ankara na Damascus.
Recep Tayyip Erdogan amebainisha kwamba, kwa sasa nchi yake inasubiri majibu ya Syria kuhusiana na takwa la kurejeshwa katika hali ya kawaida uhusiano kati ya mataifa hayo mawili jirani.
Mwezi Julai mwaka huu Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki alitoa ishara mpya ya kuanzisha tena uhusiano kati yake na serikali ya Syria kwa kutangaza kuwa huenda karibuni hivi akatuma mwaliko kwa Rais Bashar al-Assad wa kutembelea Uturuki.
Katika miaka ya hivi karibuni, na licha ya kupungua mivutano kati ya serikali nyingi za eneo hili na Syria, lakini uhusiano wa Ankara-Damascus haujarudi kama ulivyokuwa zamani. Kwa mtazamo wa serikali ya Syria, kikwazo kikubwa ni uungaji mkono wa Uturuki kwa magenge ya kigaidi yanayofanya mauaji dhidi ya raia na maafisa wa serikali nchini Syria kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.
Serikali ya Syria imekuwa ikitangaza mara kwa mara kuwa Uturuki inapaswa kukomesha kuikalia kwa mabavu ardhi ya Syria na kuacha kuunga mkono magenge ya kigaidi. Damascus inasisitiza kuwa "Makubaliano ya Adana" (1998) ndiyo makubaliano bora zaidi ya kutatua masuala yaliyopo kati ya Syria na Uturuki.