Jibu la awali la Hizbullah kwa chokochoko na uafriti wa Netanyahu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i116682-jibu_la_awali_la_hizbullah_kwa_chokochoko_na_uafriti_wa_netanyahu
Baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kiongozi mwenyewe wa utawala huo bandia Netanyahu kukataa kusitisha vita katika Ukanda wa Ghaza na badala yake kuanzisha mauaji ya kigaidi kupitia hujuma za kimtandao nchini Lebanon, hatua hiyo sio tu imekwamisha juhudi za kurejeshwa amani katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na eneo kwa jumla,
(last modified 2024-09-23T04:40:28+00:00 )
Sep 23, 2024 04:40 UTC
  • Jibu la awali la Hizbullah kwa chokochoko na uafriti wa Netanyahu

Baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kiongozi mwenyewe wa utawala huo bandia Netanyahu kukataa kusitisha vita katika Ukanda wa Ghaza na badala yake kuanzisha mauaji ya kigaidi kupitia hujuma za kimtandao nchini Lebanon, hatua hiyo sio tu imekwamisha juhudi za kurejeshwa amani katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na eneo kwa jumla,

lakini hatua ya Tel Aviv iliyofuatia baada ya hapo, ya kuzusha chokochoko mpya imewalazimisha Wanamuqawama kushadidisha na kupanua wigo wa majibu yao, bali hata kufungua ukurasa mpya wa operesheni zao.
 
Alfajiri ya kuamkia Jumapili, na baada ya kushadidi mashambulio ya hivi karibuni ya jeshi la Kizayuni kusini mwa Lebanon, Muqawama wa Kiislamu wa nchi hiyo ulilenga maeneo makubwa zaidi kuanzia kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu hadi kusini mwa Haifa kwa mashambulizi makali ya makombora na maroketi.
 
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah imetangaza kuwa imevishambulia vituo vya kijeshi vya utawala wa Kizayuni vya kampuni ya utengezaji zana za kivita ya Rafael kwa makombora ya Fadi 1 na Fadi 2.
Kombora la Fadi 1

Katika taarifa yake, Hizbullah imetangaza kuwa, operesheni hiyo ya mashambulizi imetekelezwa katika kuiunga mkono Ghaza na kutoa jibu la awali kwa mauaji ya kinyama yaliyofanywa siku ya Jumanne na Jumatano na utawala wa Kizayuni katika maeneo mbalimbali ya Lebanon.

Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti kuwa, maroketi yapatayo120 yalirushwa kutoka Lebanon; na vikosi vya zimamoto vinashughulika kuzima moto katika maeneo mbalimbali ya kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
 
Vyombo hivyo vya habari vimeongeza kuwa: Hizbullah imeelekeza mashambulizi yake kwenye maeneo na vituo vya usalama na kiuchumi; na kwa mara ya kwanza katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, yamesababisha hasara na uharibifu mkubwa hasa katika maeneo ya Haifa na Kerioth.

Kufuatia mashambulizi makubwa ya makombora ya Hizbullah ya Lebanon dhidi ya maeneo ya kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, viongozi wa utawala wa Kizayuni wamepiga marufuku kutangazwa ripoti na habari zinazohusiana na hasara na uharibifu uliosababishwa na mashambulizi hayo.

 
Mashambulizi ya Hizbullah ya Lebanon, ambayo yanafanywa kwa lengo la kuunga mkono Muqawama wa Ghaza na kujibu mashambulizi ya kinyama ya utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya raia wa kusini mwa Lebanon, yamegeuka jinamizi kwa walowezi wa Kizayuni, ambao kwa miezi kadhaa sasa wameyakimbia maeneo ya kaskazini ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, na kuyafanya maeneo hayo yaonekane kama mji wa wafu.
 
Wakati huo huo, tovuti ya habari ya Walla yenye mfungamano na duru za usalama za utawala wa Kizayuni imetangaza kuanzishwa medani mpya ya utoaji vitisho kwa wakazi wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na kuandika kuwa: wakati macho ya kila mmoja yameelekezwa angani na ardhini, inapasa jeshi la Israeli lijiandae kushtukizwa na mashambulio ambayo yanaweza kufanywa kutokea baharini.
 
Kikao cha baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni ambacho kilipaswa kufanyika Jumamosi usiku, awali kiliahirishwa kutokana na matukio ya kiusalama, lakini baadaye vyombo vya habari vya Kizayuni vikatangaza kufutwa moja kwa moja kikao hicho.
 
Katika operesheni za kigaidi ulizofanya siku ya Jumanne na Jumatano nchini Lebanon, utawala wa Kizayuni uliripua maelfu ya vifaa vya mawasiliano vya 'pager' na mifumo ya mawasiliano na kusababisha vifo vya raia wasiopungua 37 mbali na kuwajeruhi wengine wapatao 4,000.
 
Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrullah alitoa hotuba siku ya Alkhamisi na kusisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni umevuka mistari yote myekundu kwa operesheni za kigaidi ulizofanya hivi karibuni nchini Lebanon na kwa hivyo utalipa gharama kubwa.
Sayyid Hassan Nasrullah

Saa kadhaa baada ya operesheni ya kigaidi ya utawala wa Kizayuni katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut, Harakati ya Hizbullah ilitekeleza moja ya operesheni zake kubwa zaidi ya makombora dhidi ya utawala wa Kizayuni na kuyateketeza maeneo mengi.

 
Kufuatia mashambulizi makali ya Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon katika eneo la kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu hadi kusini mwa Haifa, vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimemdhihaki waziri mkuu wa utawala huo ghasibu vikisema, baada ya kuanza wimbi hilo jipya la mashambulizi ya makombora, itabidi sasa Netanyahu afikirie namna ya kuwarudisha wakazi wa Haifa majumbani mwao, kwa sababu ameshindwa pia kuwarudisha walowezi waliokimbia makazi yao kaskazini mwa ardhi zilizokaliwa kwa mabavu.
 
Hivi sasa inaonekana kuwa, utawala wa Kizayuni ukisaidiwa na kamandi kuu ya kijeshi ya Marekani Centcom unapanga kuanzisha awamu mpya ya vita katika eneo la kaskazini kwa kisingizio cha kuwarejesha walowezi hao walioyakimbia makazi yao. Madai hayo yanatolewa kama kisingizio cha kuanzisha vita katika hali ambayo, siku ya Alkhamisi ya Septemba 19, Sayyid Hassan Nasrullah alitamka kinagaubaga kuwa, njia pekee ya kuhitimisha mvutano kwenye medani ya kaskazini ni kukomeshwa vita katika Ukanda wa Ghaza na kuondoka jeshi la Kizayuni katika eneo hilo. Hii inamaanisha kwamba, ni utawala wa Kizayuni ndio wa kuamua kama mapigano yapungue au yashadidi katika eneo.
 
Japokuwa utawala huo ghasibu unalipa gharama kubwa na hasara isiyomithilika kwa kuendeleza vita, lakini inavyoonekana, Netanyahu atafadhilisha kukoleza moto wa vita hivyo ili kuokoa maisha yake ya kisiasa na kuitumbukiza serikali ya Biden kwenye changamoto ya uchaguzi ujao wa rais wa Marekani kwa madhumuni ya kutoa msukumo na msaada kwa Trump dhidi ya Harris katika kinyang'anyiro hicho.../