Viongozi wa nchi tofauti wasisitiza ulazima wa kusimamishwa vita vya Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i116808-viongozi_wa_nchi_tofauti_wasisitiza_ulazima_wa_kusimamishwa_vita_vya_gaza
Suala la Israel kuivamia Gaza na kusikitishwa viongozi wa dunia na kuendelea jinai za utawala huo ghasibu dhidi ya Wapalestina wanaoishi Gaza ni moja ya mada muhimu za hotuba za viongozi wa nchi mbalimbali katika kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.
(last modified 2024-09-26T23:05:38+00:00 )
Sep 26, 2024 23:05 UTC
  • Viongozi wa nchi tofauti wasisitiza ulazima wa kusimamishwa vita vya Gaza

Suala la Israel kuivamia Gaza na kusikitishwa viongozi wa dunia na kuendelea jinai za utawala huo ghasibu dhidi ya Wapalestina wanaoishi Gaza ni moja ya mada muhimu za hotuba za viongozi wa nchi mbalimbali katika kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.

Katika uwanja huo, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, ambaye nchi yake ni taifa la kwanza kuushtaki utawala wa kibaguzi wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kwa kufanya mauaji ya kimbari katika vita vya Gaza, amesema: "Katika kujibu mashambulizi ya Hamas, Israel inawaadhibu kwa pamoja watu wa Gaza. Wapalestina wamekuwa wakiteseka kwa zaidi ya karne moja sasa kutokana na siasa za mabavu za Israel na sisi hatutanyamaza kimya hata kidogo mbele ya siasa hizo."

Rais wa Afrika Kusini amesema kuwa njia pekee ya kumaliza mapigano na migogoro ya Asia Magharibi ni kuundwa taifa huru la Palestina. Viongozi wa nchi tofauti za dunia, hasa wa nchi za Afrika na Amerika ya Kusini, pamoja na nchi za eneo hili, katika hotuba zao kwenye vikao vya Umoja wa Mataifa, huku wakilaani jinai za Israel, wametaka kukomeshwa haraka jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya watu wasio na hatia huko Gaza na Lebanon.

Nyingi ya nchi hizo ambazo ni wahanga wa ubaguzi wa rangi na ukoloni wa nchi za Magharibi, zimekuwa zikijaribu kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni kwa miezi kadhaa sasa huku zikilaani uchokozi wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia. Katika kikao cha hivi karibuni, Rais Gustavo Petro wa Colombia, amezitaja jinai zinazoendelea huko Gaza kuwa ni mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina naye Rais Lola Da Silva wa Brazil  amesema: "Kille kilichoanza kama kitendo cha kigaidi kimegeuka kuwa adhabu ya pamoja dhidi ya watu wote wa Palestina, na haki ya kujitetea imegeuka kuwa haki ya kulipiza kisasi."

Katika hotuba yake kuhusu mgogoro wa Gaza na vita vya Israel na Hamas, Rais Masoud Pezeshkian pia amesema jamii ya kimataifa inapaswa kusimamisha mara moja ghasia na kuanzisha usitishaji vita wa kudumu haraka iwezekanavyo. Tangu tarehe 7 Oktoba mwaka uliopita, utawala wa Kizayuni umefanya mauaji makubwa ya kutisha dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi wala hatia yoyote katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, kwa uungaji mkono na msaada wa pande zote wa nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, kiasi kwamba umeua kwa umati zaidi ya Wapalestina 41,000 na kujeruhi maelfu kwa maelfu ya wengine, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wachanga.

Cyril Ramaphosa akizungumza katika kikao cha UNGA

Uchokozi huo unaendelea katika hali ambayo Gaza inakabiliwa na hali mbaya sana ya kibinadamu. Katika ripoti yake ya hivi karibuni, Amnesty International imelituhumu jeshi la Israel kwa kufanya jinai za kivita katika Ukanda wa Gaza na kutaka uchunguzi wa kimataifa ufanyike kuhusiana na suala hilo. Vilevile Shirika la Mpango wa Chakula Duniani limetahadharisha kuwa, Wapalestina milioni mbili katika ukanda huo ambao wanauawa kikatili na utawala ghasibu wa Israel, wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Ukosoaji wa siasa za utawala wa Kizayuni kimataifa umeongezeka kiasi kwamba jarida la Politico la nchini Marekani limeandika kwamba radiamali kali ya viongozi wa dunia inaashiria kuwa wamekatishwa tamaa na ukweli kuwa pande husika katika vita vya Gaza hazitaki kusitisha vita. Sambamba na hayo, wengi wameeleza kusikitishwa kwao na uzembe wa taasisi za kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa, katika kusimamisha mapigano na kurudisha amani huko Gaza. Takwa hilo la kimataifa la kutaka kusimamishwa uchokozi wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza linatolewa katika hali ambayo utawala huo wa kibaguzi si tu umeongeza uchokozi wake dhidi ya Wapalestina katika siku za hivi karibuni, bali pia umeeneza uchokozi huo hadi ndani ya ardhi ya Lebanon.

Ijapokuwa nchi nyingi za dunia hususan katika wiki za hivi karibuni zimekosoa uchokozi na siasa za jinai za utawala wa Kizayuni na kutaka zikomeshwe mara moja lakini Marekani na nchi za Magharibi zinaendelea kuunga mkono moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja na kuupa silaha za kisasa kabisa ili uendelee kuwaua kwa umati Wapalestina na Walebanon wasio na hatia.

Licha ya kuwa washiriki wa vikao vya Umoja wa Mataifa wameendelea kukosoa na kulaani uchokozi wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina na Walebanon, lakini ni wazi kuwa Israel inaendeleza uchokozi wake huo kwa uungaji mkono kamili wa waitifaki wake wa Magharibi hususan Marekani na hivyo kupuuza kabisa matakwa ya jamii ya kimataifa kuhusu suala hilo.