Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina: Acheni kuipatia Israel silaha
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amehutubia Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, na kutoa wito wa kutoupatia silaha utawala wa Kizayuni wa Israel.
Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuacha kuipatia silaha Israel: "Acheni uhalifu huu. Acheni sasa. Acheni kuua watoto na wanawake. Acheni mauaji ya halaiki. Acheni kupeleka silaha kwa Israel. Janga hili haliwezi kuendelea. Dunia nzima inahusika na kile kinachotokea kwa watu wetu huko Gaza na Ukingo wa Magharibi."
Mahmoud Abbas amelaani mashambulizi ya utawala haramu wa Israel na kuelezea vitendo vya Israel katika maeneo ya Palestina kama "mauaji ya halaiki". Aidha amesema katika hotuba yake hiyo kwamba, Wapalestina wanakabiliwa na moja ya uhalifu mbaya zaidi wa zama hizi na kusisitiza kuwa Israel inaendesha uhalifu wa vita kamili na mauaji ya kimbari.
“Huu wazimu inabidi ukome. Dunia nzima inawajibika kwa kile ambacho watu wetu wanateseka huko Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan,” aliongeza kiongozi huyo wa Palestina, huku akishangiliwa sana alipopanda jukwaani.
Kadhalika Mahmoud Abbas amebainisha kuwa, Israel, ambayo inakataa kutekeleza maazimio ya Umoja wa Mataifa, haistahiki kuwa mwanachama wa taasisi hiyo ya kimataifa na kuitaja Marekani kuwa mshirika wa Israel katika mauaji na jinai za Tel Aviv dhidi ya Wapalestina.
Rais Mamlaka ya Ndani ya Palestina amekosoa vikali hatua ya Marekani ya kutumia kura ya veto kuingikia kifua Israel na wakati huo huo kukwamisha juhudi za Palestina kutambuliwa kama mwanachama kamili wa Umoja wa Mataifa.