Rais Erdogan: Israel ni Shirika la Kigaidi la Kizayuni
Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amekosoa vikali mashambulio ya kigaidi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon na Gaza na kuitaja Israel kuwa ni "shirika la kigaidi la Kizayuni".
Erdoğan ambaye alikuwa akizungumza mbele ya wabunge wa chama tawala cha Justice and Development, kwa mara nyingine tena amekosoa madola ya Magharibi hasa Marekani kutokana na hatua yao ya kutoa himaya na uungaji mkono kwa Israel.
Rais wa Uturuki pia ameonya kwamba mzozo kati ya Iran na Israel umeongeza hatari ya vita vya kikanda.
Bwana Erdogan, ambaye ana historia ndefu ya ukosoaji mkali wa Israel, hapo awali alimwita Benjamin Netanyahu "mchinjaji wa Gaza" na kumlinganisha yeye na serikali yake na Hitler na serikali ya Ujerumani ya Nazi.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, ripoti zinaonyesha kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel unatumia silaha zilizopigwa marufuku kushambulia maeneo ya raia ya Lebanon na Ukanda wa Gaza.
Baada ya kuanza kwa Oparesheni ya Kimbunga cha Al-Aqswa, na mashambulizi ya jeshi la Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza, zilichapishwa ripoti kuhusu matumizi ya silaha za maangamizi umati huko Ukanda wa Gaza. Ripoti hizo zinaonyesha kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel pia umetumia mabomu yenye madini ya urani iliyohafifishwa katika mashambulizi yake ya hivi karibuni dhidi ya Lebanon.