Kuendelea juhudi za Iran za kutanua ushirikiano wa kikanda
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i117394-kuendelea_juhudi_za_iran_za_kutanua_ushirikiano_wa_kikanda
Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameendelea na safari yake ya kuzitembelea nchi za eneo hili la Asia Magharibi ambapo baada ya kuitembelea Saudia ameitembelea pia Qatar katika jitihada za kuleta ushirikiano mkubwa zaidi wa kieneo na kutafuta njia za kukomesha jinai za Israel huko Palestina na Lebanon.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Oct 11, 2024 11:13 UTC
  • Kuendelea juhudi za Iran za kutanua ushirikiano wa kikanda

Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameendelea na safari yake ya kuzitembelea nchi za eneo hili la Asia Magharibi ambapo baada ya kuitembelea Saudia ameitembelea pia Qatar katika jitihada za kuleta ushirikiano mkubwa zaidi wa kieneo na kutafuta njia za kukomesha jinai za Israel huko Palestina na Lebanon.

Wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alitembelea Lebanon na Syria na kukutana na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hizo. Jumatano ya juzi aliekea Saudi Arabia ambako alionana na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Faisal bin Farhan Aal Saud na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia, Mohammad bin Salman na kujadiliana nao mambo yanayohusu pande mbili, ya kieneo na ya kimataifa. 

Jana Alkhamisi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliwasili Doha, mji mkuu wa Qatar na kuonana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Aal Thani na kujadiliana naye mambo muhimu yanayozihusu nchi mbili. 

Nchi mbili za Iran na Qatar zina uhusiano mzuri katika mambo mengi

 

Mambo yaliyopewa kipaumbile kikuu katika ziara zote hizo za Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ni jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza na Lebanon. Sambamba na kulaani vikali jinai hizo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafanya jitihada za kuhakikisha wananchi wa Ghaza na Lebanon wanasaidiwa na kuungwa mkono na imekuwa muda wote ikihimiza wajibu wa nchi za Kiislamu za eneo hili kuungana na kuilazimisha Israel ikomeshe jinai zake huko Ghaza na Lebanon. 

Qatar ni miongoni mwa nchi za Kiislamu ambazo tangu Israel ilipoanza kufanya mauaji ya kimbari huko Ghaza mwaka mmoja uliopita, imekuwa ikifanya juhudi kubwa za kutaka kukomeshwa jinai hizo. Qatar imewekeza nguvu zake katika kuhakikisha mazungumzo ya kukomesha vita dhidi ya wananchi wa Ghaza yanafikiwa na mara zote imekuwa ikijitolea katika mambo mbalimbali na kutumia fedha nyingi kuhakikisha Israel inakomesha jinai zake, lakini muda wote inakwamishwa na utawala wa Kizayuni.

Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje akaamua kutembelea Qatar na kuzungumza na Waziri Mkuu wa nchi hiyo ili kuunganisha nguvu katika juhudi za kidiplomasia za Doha za kuwapunguzia masaibu wananchi wa Ghaza na Lebanon. Nchi mbili za Iran na Qatar zina mtazamo mmoja kwamba utawala wa Kizayuni ni tishio kwa usalama wa eneo hili zima na kwamba jinai zake hizo hazitoishia tu Palestina na Lebanon. 

Mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia

 

Suala jingine ambalo limepewa umuhimu mkubwa katika ziara ya kikanda ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ni kuimarisha ushirikiano baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchi za eneo hili zikiwemo Qatar na Saudi Arabia. Uhusiano wa Iran na Qatar ni mara chache sana kukumbwa na mivutano. Nchi hizi mbili zinakamilishana na kuwepo ushirikiano mkubwa baina yao ni jambo la dharura kwani zina mambo mengi ya pamoja ikiwa ni pamoja na kuwa kwao jirani. Nchi hizi mbili zina mpaka wa pamoja na katika upande wa kisiasa pia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Qatar ni kati ya nchi zinazofanya juhudi kubwa za kuaminiana na kutokuwa na misuguano ya kisiasa.

Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana baada ya kuonana na Waziri Mkuu wa Qatar, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akagusia siasa za ujirani mwema baina ya Tehran na Doha na udharura wa kupewa kipaumbele masuala yote yatakayopelekea ujirani huo uzidi kuwa mwema, imara na wenye ushirikiano wa pande zote.