Hizbullah yashambulia Tel Aviv kwa ndege zisizo na rubani
Harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon imetekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi katika viunga vya mji wa Tel Aviv ulio katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kwa kutumia idadi kubwa ya ndege za kivita zisizo na rubani aina ya kamikaze.
Katika taarifa siku ya Jumamosi, Hizbullah ilisema ilifanya operesheni hiyo "kuunga mkono watu wetu wa Kipalestina walio imara katika Ukanda wa Gaza na mapambano yao ya kijasiri na vile vile kwa ajili ya ulinzi wa Lebanon na watu wake."
Hizbullah ilianzisha mamia ya mashambulizi hayo ya kulipiza kisasi dhidi ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu tangu mwezi Oktoba mwaka jana, wakati utawala wa Israel ulipoanza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza sambamba na kushadidisha mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya Lebanon. Tokea Oktoba mwaka jana hadi sasa Israel imeua Wapalestina zaidi ya 42,100 na zaidi ya watu 2,000 wa Lebanon, wengi wakiwa ni wanwake, watoto na raia wa kawaida.
Jana pia Hizbullah ilitekeleza operesheni kadhaa dhidi ya jeshi la Israel ambapo katika moja ya operesheni hizo iliwalenga wanajeshi wa Israel waliokuwa wakijaribu kujipenyeza katika ardhi ya Lebanon kutoka upande wa eneo la Ramia na kuwasabishia hasara kubwa.
Harakati hiyo imeapa kuendeleza mashambulizi dhidi ya ngome za utawala haramu wa Israel hadi utawala huo utakapositisha uchokozi wake dhidi ya Gaza na Lebanon.