Hamas: Israel imeshindwa kusambaratisha muqawama
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i117448-hamas_israel_imeshindwa_kusambaratisha_muqawama
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (muqawama) Palestina, Hamas, imesema utawala wa haramu wa Israel umeshindwa kusambaratisha wanamuqawama shupavu katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2024-10-13T03:29:25+00:00 )
Oct 13, 2024 03:29 UTC
  • Hamas: Israel imeshindwa kusambaratisha muqawama

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (muqawama) Palestina, Hamas, imesema utawala wa haramu wa Israel umeshindwa kusambaratisha wanamuqawama shupavu katika Ukanda wa Gaza.

Osama Hamdan, mwakilishi mkuu wa Hamas nchini Lebanon, aliyasema hayo katika mahojiano na televisheni wa Al Jazeera wa Qatar siku ya Jumamosi.

Akizungumzia kushindwa kwa utawala wa Kizayuni kukabiliana na muqawama, amesema, "Utawala wa Kizayuni haukabiliana na wanamuqawama badala yake unalenga kuua raia. Utawala ghasibu unaua raia kwa kisingizio cha kukabiliana na muqawama."

Afisa wa Hamas pia ametoa maoni yake kuhusu mpango wa utawala wa Kizayuni  baada ya vita vya Gaza ambapo inaripotiwa kuwa Israel inapanga kukabidhi usimamizi wa eneo hilo kwa 'taasisi za Palestina" ambazo bado hazijulikani ambapo utawala huo utasimamia usalama wa eneo hilo.

Afisa huyo wa Hamas amesema mpango huo ni njama ya Israel ya kukoloni eneo la Gaza huku akisisitiza kuwa harakati hiyo inataka eneo hilo liwe na utawala wa mpito wa serikali ya umoja wa kitaifa au kamati ya kusimamia eneo hilo.

Amesisitiza tena kwamba ukatili wa Israel hautaufikisha popote utawala huo, na kuongeza kuwa, "suluhisho lipo kwa Wapalestina kurejeshewa haki zao na waweze kuanzisha serikali wanayoitaka."