Jihadul Islami: Marekani inahusika na mauaji ya kimbari kaskazini mwa Gaza
(last modified 2024-10-21T02:46:20+00:00 )
Oct 21, 2024 02:46 UTC
  • Jihadul Islami: Marekani inahusika na mauaji ya kimbari kaskazini mwa Gaza

Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imesema kuwa Marekani inahusika na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

Televisheni ya al Mayadeen imeripoti kuwa, Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imetoa taarifa na kuashiria hatua ya Marekani ya kuwapa silaha Wazayuni maghasibu na kusisitiza kuwa  utawala wa Kizayuni unatekeleza jinai mpya kaskazini mwa Gaza sambamba na kutangazwa kwa mpango mpya wa baraza la mawaziri la utawala huo, kwa jina la "Mpango wa Majenerali" kwa lengo la kuangamiza uhai wa eneo hilo.  

Jihadul Islami imebainisha kuwa utawala wa ghasibu wa Israel umewazingira raia wa Kipalestina karibu elfu nne huko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza huku ukizishambulia kwa makusudi hospitali katika ukanda huo. 

Mauaji ya kimbari yanayotekelezwa sasa na utawala wa Kizayuni mbele ya macho ya walimwengu ni makubwa zaidi ya yale yaliyofanywa na utawala huo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. 

Mauaji ya kimbari ya Israel Ukanda wa Gaza 

Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa, hadi sasa watu 42,603 wameuawa shahidi  na 99,795 kujeruhiwa katika Ukanda wa Gaza tangu kuanza oparesheni ya Kimbunga cha al Aqsa Oktoba 7 mwaka jana.