Jul 23, 2016 16:30 UTC
  • Jeshi na wananchi Yemen wajiweka tayari kukabiliana na Saudia

Mkuu wa Kamati ya Mapinduzi nchini Yemen ameelezea habari ya kujiweka tayari kwa kila upande jeshi na harakati za kujitolea za wananchi kwa ajili ya hujuma zozote za Saudia.

Muhammad Ali al-Houth aliyasema hayo katika mazungumzo yake na makamanda wanaoongoza mapambano katika uwanja wa vita na kusema kuwa, kwa bahati mbaya mazungumzo ya amani ya Yemen yanayoendelea nchini Kuwait hayaendi njia sahihi. Amesema kufuatia hali hiyo jeshi na harakati za wananchi zimeamua kujiweka tayari kwa kila upande kwa ajili ya kukabiliana na hujuma tarajiwa za adui.

Wapiganaji wa harakati ya al Houthi

Al-Houth amesisitiza kuwa, kuweka masharti kama njia ya kuhitimishwa mgogoro, hakuwezi kumaliza matatizo na kwamba kufanya mazungumzo na upande wa pili na kuukinaisha kwa hoja ndiko kunakoweza kuhitimisha matatizo ya Yemen na si vinginevyo. Vilevile amesema kuwa ni jambo lisilowezekana kwa watu wanaotenda jinai dhidi ya Yemen na taifa hilo kukabidhiwa silaha. Kadhalika mkuu wa Kamati ya Mapinduzi nchini Yemen amesisitiza kuwa, kama ambavyo jeshi na harakati za wananchi nchini humo zilivyoweza kusimama kidete katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu dhidi ya muungano wa nchi vamizi unaoongozwa na Saudia, pia zina uwezo wa kuendelea kusimama imara na kupambana na adui kwa maslahi ya taifa hilo.

Tags