Apr 11, 2016 08:16 UTC
  • Houthi: Tutaheshimu makubaliano ya usitishaji vita Yemen

Harakati ya Houthi ya Yemen imesema itaheshimu makubaliano ya usitishaji vita nchini humo.

Katika barua iliyoituma kwa Umoja wa Mataifa, harakati hiyo imesema itaheshimu makubaliano ya kusitisha mashambulizi yote yakiwemo ya ardhini, angani na baharini kote nchini Yemen.

Muhammed Ali al-Makdashi, mmoja wa maafisa waandamizi wa Kihouthi ameliambia shirika la habari la AFP kuwa: “Tutaheshimu kikamilifu makubaliano hayo na tunatumai kwamba hatua hiyo itakuwa kwa maslahi ya Wayemen wote ya kupatikana amani ya kudumu nchini humo.

Hii ni katika hali ambayo, ndege za kivita za Saudia jana Jumapili ziliendelea kudondosha mabomu katika maeneo kadhaa ya mji mkuu San’aa. Usitishwaji vita umetangazwa na mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Yemen, Ismail Ould Cheikh Ahmed kama njia ya kutuliza hali ya mambo kabla ya mazungumzo ya amani yanayoanza tarehe 18 Aprili nchini Kuwait.

Hadi hivi sasa watu wasiopungua 9,400 wameshauawa na wengine zaidi ya 16,000 kujeruhiwa tangu Saudia na washirika wake walipoanzisha mashambulio na uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka jana kwa lengo la kuisambaratisha Harakati ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wa utawala wa Aal Saud, Rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kuitoroka nchi Abd Rabbuh Mansur Hadi.

Mashambulio hayo yameshindwa kufikia malengo hayo zaidi ya kuangamiza na kusababisha hasara kubwa kwa miundombinu ya Yemen, zikiwemo hospitali, shule, misikiti na turathi za kihistoria za nchi hiyo.

Tags