Oct 19, 2016 07:44 UTC
  • UN: Saudia ikomeshe mashambulizi yake Yemen na kuheshimu usitishaji vita

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen ameitaka Saudia kukomesha mashambulizi yake nchini humo mara moja kupitia makubaliano ya usitishaji vita.

Ismail Ould Cheikh Ahmed ameyasema hayo huku akizitaka pande husika katika mapigano nchini Yemen hususan Saudia, kuheshimu makubaliano ya usitishaji vita wa masaa 72 ili kuanza shughuli za kuwafikishia misaada ya kibinaadamu raia wa nchi hiyo.

Sehemu ya jinai za Saudia nchini Yemen

Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, makubaliano hayo ya usitishaji vita na utekelezwaji wake, ni njia ya kuanza upya harakati za tume za upatanishi na kuongeza kuwa, hatua hiyo itasaidia pia kufikiwa usitishaji vita wa kudumu nchini Yemen. Ismail Ould Cheikh Ahmed ametaka kuendelezwa bila masharti wala kizuizi shughuli za ugawaji misaada ya kibinaadamu kwa raia wa Yemen.

Viongozi wa Saudia wakimzika mmoja wa askari wao aliyeangamizwa Yemen

Kadhalika amezitaka pande husika katika eneo na kimataifa, kushiriki katika utekelezwaji wa makubaliano ya usitishaji vita. Jumatatu iliyopita, Ismail Ould Cheikh Ahmed alitangaza kuwa, makundi ya kisiasa na asasi za kiraia nchini Yemen zimeahidi kuheshimu usitishaji vita utakaoanza alfajiri ya kesho Alkhamis ambapo kwa hatua ya kwanza utadumu kwa kipindi cha masaa 72. Makubaliano ya usitishaji vita nchini Yemen yamefikiwa mara kadhaa huku Saudia ikiwa ya kwanza kuyavunja kwa kushambulia kinyama raia wasio na hatia wa nchi hiyo.

Tags