WFP: Hatutachukua jukumu la UNRWA Gaza
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP limetangaza kuwa, haliwezi kutumika kama mbadala wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya kiutu kwa Wakimbizi wa Kipalestina katika Mashariki ya Kati (UNRWA) huko Gaza.
Mkuu wa ofisi ya WFP mjini Berlin Martin Frick ya amesema hayo alipozungumza na vyombo vya habari vya Ujerumani.
Frick alisema, UNRWA ndio uti wa mgongo wa utoaji wa misaada ya chakula, ulinzi na matibabu kwa watu wa Ukanda Gaza wanaokabiliwa na hali mbaya kutokana na vita.
Hivi karibuni utawala haramu wa Israel ulitangaza kulipiga marufuku shirika hilo la Umoja wa Mataifa na kusema kuwa Israel yenyewe itachukua jukumu hilo pamoja na mashirika mengine katika kuratibu na kusambaza misaada katika ukanda wa Gaza.
WFP imesema kulipiga marufuku shirika la UNRWA kutahatarisha zaidi maisha ya watu ambao kwa sasa wanajaribu kuishi kwa kutumia rasilimali zao za mwisho.
Wakati huo huo, kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo hali ya usalama na kibinadamu huko Ukanda wa Gaza inavyozidi kuzorota huku raia na hata wafanyakazi wa kutoa misaada wakisalia wamepigwa butwaa kwani mashambulizi kutoka Israeli yanaendelea kila uchao.