Qatar yaonya kuhusu kupigwa marufuku UNRWA
Serikali ya Qatar imeonya kuhusiana na hatua ya kupigwa marukufu shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) na kusisitiza udharura wa kuheshimiwa haki za Wapalestina.
Onyo hilo limetolewa na Sheikh Jassim bin Abdulaziz Al-Thani mmoja wa wajumbe wa ujumbe wa kudumu wa Qatar katika Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, msimamo wa Doha kuhusu shughhuli za UNRWA uko thabiti.
Afisa huyo wa Qatar katika Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa, nchi yake itaendelea kutoa himaya na uungaji mkono wake wa kidiplomasia na kifedha kwa taasisi hiyo.
Aidha ameonya kuwa kupigwa marufuku shughuli za UNRWA kutasababisha madhara hatari ya kibinadamu na kisiasa, hasa kunyimwa huduma muhimu mamilioni ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Hivi karibuni Knesset (bunge) ya utawala wa Kizayuni ilipitisha sheria dhidi ya UNRWA wiki iliyopita kwa kuidhinishwa na wawakilishi 92 dhidi ya upinzani wa wawakilishi 10, ambayo inapiga marufuku shughuli za UNRWA katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na utawala huo pandikizi tangu mwaka 1948.
Wakati huo huo, Kamishna Mkuu wa UNRWA ameonya kwamba, endapo sheria ya kupiga marufuku shughuli za UNRWA itatekelezwa basi kutatokea maafa makubwa yakiwemo katika sekta ya elimu.