HAMAS yajibu vitisho alivyotoa Trump kuhusu mateka wa Kizayuni wanaoshikiliwa Ghaza
Dec 04, 2024 06:42 UTC
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imetoa jibu kwa ujumbe wa vitisho uliotolewa na rais mteule wa Marekani kuhusu mateka wa Kizayuni wanaoshikiliwa katika Ukanda wa Ghaza na kusisitiza kuwa, ni bora Trump atume salamu zake hizo kwa Netanyahu.
Siku ya Jumatatu Trump aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii unaojulikana kwa jina la "Truth Social" kwamba, ikiwa mateka wa utawala wa Kizayuni hawataachiliwa kabla ya sherehe za yeye kuapishwa kuwa rais mnamo Januari 20, 2025, itazuka jehanamu Magharibi mwa Asia na kwa wale waliotenda alichokiita jinai dhidi ya ubinadamu.
Basem Naeem, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas amesema, ujumbe wa Donald Trump inapasa utumwe kwa Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni, kwa sababu yeye na baraza lake la mawaziri lenye misimamo mikali ndio wanaozuia kufikiwa makubaliano ya kusimamisha vita.
Bassem Naim ameongeza kuwa, Netanyahu na baraza lake la mawaziri wanapaswa kukomesha mchezo wao wa kiafriti wa kutumia mazungumzo kama wenzo wa kufanikishia maslahi yao ya kisiasa ya itikadi zao za binafsi.
Mjumbe huyo wa Hamas amesisitiza kuwa, tangu yalipoanza mauaji ya kimbari ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza, Hamas imekuwa ikifanya juuchini ili kuweza kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita wa kudumu na ya kubadilishana mateka, lakini baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni limezuia kutekelezwa takwa hilo la makundi ya Muqawama.
Familia za mateka wa Kizayuni nazo pia zinamtaka Netanyahu afanikishe kuachiwa huru mateka wa Kizayuni walioko mikononi mwa Muqawama kupitia mapatano na Muqawama huo wa Palestina bila kupoteza muda, na kukomesha mashambulizi yasiyo na faida dhidi ya Ukanda wa Ghaza, ambayo mbali na Wapalestina yanaua pia mateka hao wa Israel../
Tags