Mamia ya maelfu ya Wayemen wafanya maandamano ya kuiunga mkono Palestina
Mamia ya maelfu ya wananchi wa Yemen kwa mara nyingine tena wamemiminika barabarani kufanya maandamano makubwa ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kuupinga utawala wa Kizayuni wa Israel.
Vyombo vya habari vimeripoti kwamba, kama ilivyokuwa Ijumaa iliyopita, wananchi wa Yemen wamefanya maandamano makubwa leo pia katika mikoa ya Saada, Rima, Ma'rib na baadhi ya maeneo mengine ya nchi hiyo kwa ajili ya kuwaunga mkono Wapalestina na harakati ya Muqawama chini ya kaulimbiu ya "Tuko pamoja na Ghaza, Jihadi na Uhamasishaji, Tuko imara kuzuia uchokozi wowote n.k."
Wananchi na wanajeshi wa Yemen wanaendesha mapambano bega kwa bega na Wapalestina tangu utawala ghasibu wa Israel ulipoanzisha mashambulizi ya kikatili kwenye Ukanda wa Ghaza na kuua Wapalestina wasio na ulinzi. Taifa imara la Yemen limetangaza kuwa litaendelea kupambana na Wazayuni na washirika wao hadi mashambulio ya kikatili dhidi ya Wapalestina yatakapokomeshwa.
Kwa upande wake, Jeneral Yahya Saree, Msemaji wa Jeshi la Yemen amesisitiza katika taarifa yake ya Alkhamisi jioni kwamba, jeshi la nchi hiyo limejipanga kwa ajili ya mapambano ya muda mrefu dhidi ya utawala wa Kizayuni kwa shabaha ya kuendesha Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, kuilinda Yemen na kuwasaidia wananchi wanaodhulumiwa wa Ukanda wa Ghaza.
Kwa mujibu wa tangazo la karibuni kabisa la Wizara ya Afya ya Palestina ya Ukanda wa Ghaza, Wapalestina 45,097 wameshauawa shahidi na 107,244 wameshajeruhiwa kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel kwenye ukanda huo tangu Oktoba 7, 2023.