Kushadidi mapigano kaskazini na kusini mwa Yemen
Sambamba na kudhoofika mazungumzo ya amani baina ya makundi ya Yemen, mapigano yanaripotiwa kushadidi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Ripoti zinaonesha kuwa, katika mapigano ya siku ya Jumatatu baina ya wavamizi ambao ni wafuasi wa Saudi Arabia na vikosi vya wananchi vikishirikiana na jeshi katika maeneo ya mpakani mwa mkoa wa kaskazini wa Hajjah makumi ya wanajeshi wa Saudia na mamluki wao wameuawa na kujeruhiwa. Brigedia Jenerali Luqman msemaji wa jeshi la Yemen amethibitisha kutokea mapigano makali katika maeneo ya kaskazini mwa Yemen yaliyoko jirani na mipaka ya Saudia na kubainisha kwamba, endapo mashambulio ya maadui hayatapungua, jeshi na vikosi vya wananchi wa Yemen vitaanzisha duru mpya ya mashambulio dhidi ya ngome za maadui wavamizi pamoja na mamluki wao.
Msemaji wa jeshi la Yemen amesema pia kuwa, katika mapigano ya hivi karibuni ndege moja ya kijeshi na mabuldoza kadhaa ya wavamizi yaliangamizwa katika maeneo ya kaskazini mwa Yemen huku wanajeshi kadhaa mamluki nao wakiuawa katika mapigano hayo.
Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia imethibitisha kuuawa na kujeruhiwa makumi ya wananchi wa nchi hiyo katika mapigano yao na jeshi la Yemen pamoja na kamati za wapiganaji za kujitolea za Wayemen huko katika eneo la Najran. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia imedai kwamba, vikosi vyake vimefanikiwa kudhibiti kituo kimoja cha kijeshi katika eneo la mpaka wa nchi mbili hizo.
Kanali ya Televisheni ya al-Masira imetangaza kwamba, raia kadhaa wameuawa na kujeruhiwa kufuatia mashambulio ya anga ya ndege vamizi za Saudia katika mkoa wa Hajjah ulioko kaskazini na Taiz uliopo kusini mwa Yemen. Aidha mashambulio hayo yamesababisha hasara kubwa.
Mapigano yanashadidi nchini Yemen katika hali ambayo, mazungumzo ya amani baina ya makundi hasimu nchini Yemen hadi sasa hayajawa na natija ya maana. Wiki iliyopita ambapo Kuwait ilikuwa mwenyeji wa mazungumzo ya amani ya Yemen ilizipatia muda wa siku 15 pande hasimu nchini Yemen ziwe zimefikia makubaliano la sivyo ziondeke nchini humo.
Pamoja na hayo Muhammad Abdul Salaam, mkuu wa timu ya mazungumzo ya Harakati ya wananchi ya Ansarullah ya Yemen amesema katika mazungumzo ya Kuwait kwamba, timu hiyo inaheshimu muda wa wiki mbili uliotolewa na serikali ya Kuwait lakini inaamini kwamba, muda huo unapaswa kuongezwa.
Amesema, mashinikizo ya Saudia katika mazungumzo ya kuwait ndicho kikwazo kikuu cha kupiga hatua mazungumzo hayo.
Mashambulio ya Saudia ikishirikiana na baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo yalianza mwezi Machi mwaka jana kwa lengo la kumrejesha madarakani Abd Rabbuh Mansur Hadi, Rais wa zamani wa Yemen aliyetangaza kujiuzulu na kukimbia nchi. Hadi sasa maelfu ya wananchi wa Yemen, wakiwemo wanawake na watoto wadogo wameshauawa huku asilimia kubwa ya miundombinu ikiharibiwa.