Jinai za Israel zinaendelea: Wapalestina wengine 15 wauawa shahidi
Wapalestina wengine 15 wameuawa shahidi katika jinai ya hivi punde ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika ukanda wa Gaza.
Duru za ndani zimetangaza kuwa, ndege za kivita za Israel zilishambulia maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza mara mbili, na kupelekea Wapalestina wengine 15 kuuawa shahidi wengine 50 kujeruhiwa.
Mashambulio na mauaji ya utawala wa Kizayuni wa Israel yanaendelea kwa himaya na uungaji mkono kamili wa maadola ya magharibi hususan Marekani inayojidai kuwa polisi wa dunia na kinara wa kutetea haki za binadamu.
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umetangaza jana katika ripoti yake kwamba idadi ya mashahidi wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza imeongezeka na kufikia zaidi ya watu 45,000 tangu Oktoba 7, 2023.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa, kati yao zaidi ya watoto 13,000 na zaidi ya wanawake 7,000, huku takriban watu 108,000 pia wakijeruhiwa.
Katika ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa kuna onyo kuhusu kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, hali ambayo inaweza kuongeza maafa ya binadamu katika eneo hilo.
Wakati huo huo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limetangaza kuwa, kila baada ya saa moja mtoto mmoja anauawa huko Gaza.