HAMAS: Tumewalazimisha wavamizi kusimamisha uvamizi na uchokozi wao
Jan 19, 2025 11:41 UTC
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS imesisitiza kuwa: Adui Mzayuni ameshindwa kufikia malengo yake na kulazimika kusimamisha uchokozi wake.
Hamas imeeleza katika taarifa: "licha ya njama za waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu za kurefusha vita na kufanya jinai zaidi, tumewalazimisha wavamizi kusimamisha uchokozi wao na kurudi nyuma".
Taarifa ya Hamas imeendelea kueleza kwamba: "adui ghasibu ameshindwa kufikia malengo yake ya kichokozi katika kuishambulia Ghaza na mafanikio pekee aliyopata ni kufanya anuai za jinai zinazouaibisha utu na ubinadamu".
Harakati hiyo ya Muqawama wa Palestina imesema: Mapigano ya Kimbunga cha Al-Aqsa sio tu yaliakisi mshikamano wa taifa adhimu la Palestina na Muqawama na kukabiliana na umaluuni wa adui, lakini ulionyesha pia kwamba damu ya vizazi vya Palestina haitapotea bure na mwishowe askari wa adui wataadhibiwa tu.
Taarifa ya harakati ya Hamas imemalizia kwa kusema, sasa ni wakati wa kuhitimishwa mzingiro, kufikishwa misaada kwa wananchi wa Palestina, kuponywa majeraha yao, kuwarejea wakimbizi na kuijenga upya Ghaza.../
Tags