Matokeo ya usitishaji vita vya Gaza kwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i121814-matokeo_ya_usitishaji_vita_vya_gaza_kwa_maeneo_yanayokaliwa_kwa_mabavu
Jeshi na baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni wamekabiliwa na hali mbaya kutokana na matokeo ya usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-01-24T00:02:29+00:00 )
Jan 24, 2025 00:02 UTC
  • Matokeo ya usitishaji vita vya Gaza kwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu

Jeshi na baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni wamekabiliwa na hali mbaya kutokana na matokeo ya usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza.

Kujiuzulu kwa makamanda wa jeshi la utawala wa Kizayuni na hatua za wapinzani za kutaka kumuondoa madarakani Waziri Mkuu wa utawala huo Benjamin Netanyahu katika siku za hivi karibuni yamekuwa matokeo ya kimsingi ya usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza.

Mkuu wa Jeshi la Israel Herzi Halevi amesema kuwa, amekabidhi barua yake ya kujiuzulu kwa Waziri wa Vita kutokana na kushindwa kutabiri na kukabiliana na operesheni za makundi ya muqawama ya Palestina tarehe 7 Oktoba 2023. Hata hivyo Halevi ataendelea kubakia katika wadhifa huo hadi Machi 6.  Katika barua yake ya kujiuzulu Herzi Halevi aliandika, "malengo yote ya vita" ya jeshi la utawala huu hayajafikiwa.

Yaron Finkelman, kamanda wa eneo la kusini la jeshi la Wazayuni, pia aliandika katika barua yake ya kujiuzulu: Pigo la Oktoba 7 litabakia katika akili yangu katika maisha yangu yote. Kufuatia kushindwa kijeshi na ukosoaji mkubwa wa utendaji wa jeshi la Israel katika vita dhidi ya Gaza, Yifat Yerushalmi, Mkuu wa Mashtaka ya kijeshi na masuala ya kisheria wa jeshi la utawala huo aliyekuwa akishikilia wadhifa wa Brigedia Jenerali alijiuzulu wadhifa wake huo.

Harakatii za wapinzani wa Baraza la Mawaziri la Benjamin Netanyahu pia zimeongezeka na kutaka waziri mkuu wa utawala huo na wajumbe wake wa baraza la mawaziri kujiuzulu, pamoja na kuundwa kwa kamati rasmi ya uchunguzi kuchunguza kushindwa kwa Oktoba 7, 2023.

Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel

 

Baada ya Halevi kutangaza kujiuzulu, viongozi wa upinzani walimkosoa Waziri Mkuu Netanyahu na kumtaka yeye na baraza lake la mawaziri kujiuzulu.  Yair Lapid, mkuu wa vuguvugu la upinzani la utawala wa Kizayuni, aliandika kwenye akaunti yake kwenye mtandao wa kijamii wa "X": "Ni wakati wa kukubali kuwajibika na waziri mkuu na wajumbe wa baraza lake la mawaziri la maafa wanapaswa kujiuzulu kwa pamoja."

Avigdor Lieberman, mkuu wa chama cha Yisrael Beiteinu, pia aliandika kwenye akaunti yake kwenye mtandao wa kijamii wa "X" kwamba "baada ya kujiuzulu kwa mkuu wa jeshi, ninamtaka Waziri Mkuu na wajumbe wa baraza la mawaziri la usalama kukubali kuwajibika na kurudi majumbani mwao."

Chama cha Democrats, kinachoongozwa na Yair Golan, mmoja wa viongozi wa  upinzani, pia kilisema katika akaunti yake kwenye mtandao wa kijamii wa "X" kwamba "Netanyahu, ni zamu yako sasa."

Utawala wa Kizayuni kwa uungaji mkono wa Marekani ulianzisha vita vikali dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza kuanzia tarehe 7 Oktoba 2023 na matokeo yake, pamoja na uharibifu mkubwa na njaa mbaya, zaidi ya Wapalestina 47,000 waliuawa shahidi na wengine zaidi ya 110,000 walijeruhiwa, wengi wao wakiwa wanawake na ni watoto.

Hatimaye, baada ya miezi 15 ya uchochezi wa kikatili wa vita na kutoweza kufikia malengo yake, yaani, kuachiliwa kwa wanajeshi wake waliokuwa mateka kupitia vita vya ardhini, kuisambaratisha Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, na kuondolewa uwezo wa kijeshi wa Ukanda wa Gaza wa kutumia makombora, Jumatano, Januari 15, 2025, Serikali ya Qatar ilitangaza kupatikana mafanikio ya juhudi za kusimamisha mapigano katika Ukanda wa Gaza kati ya pande za Palestina na Israel, na kwamba utekelezaji wa makubaliano hayo ulianza kutekelezwa Jumapili, Januari 19 ili kuhitimisha miezi zaidi ya15 ya vita vya kinyama na mauaji ya kimbari ya ya jeshi la Kizayuni.

 

Awamu ya kwanza ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Hamas na utawala wa Kizayuni itadumu hadi wiki 6.   Katika hatua hii, utekelezaji wa makubaliano katika hatua ya pili na ya tatu itajadiliwa. Makubaliano haya yalifikiwa kwa upatanishi wa Qatar, Misri na Marekani na duru kadhaa za mazungumzo zilifanyika Cairo na Doha.

Kuporomoka kisiasa na kijeshi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu imekuwa moja ya matokeo ya usitishaji mapigano. Mgogoro na hitilafu katika jeshi la utawala wa Kizayuni pia unaendelea huku mamlaka za utawala wa Kizayuni zikikiri kushindwa jeshi la utawala huo dhidi ya muqawama wa Palestina.

Matukio mawili makubwa na ya kimsingi yamekuwa na taathira kufuatiwa usitishaji vita wa Gaza kwa muundo wa jeshi la utawala wa Kizayuni na baraza la mawaziri la utawala huo ghasibu. Mosi, kujiuzulu kwa makamanda mashuhuri wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni kunaonyesha kutoridhishwa kwao na matokeo ya vita na utendaji wa baraza la mawaziri.

Suala jingine ni hitilafu kubwa kati ya Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada na wajumbe wengine wa baraza la mawaziri la Netanyahu kuhusu kuendelea vita vya Gaza. Wazayuni wenye misimamo ya kuchupa mipaka wanaunga mkono kuendelea vita huko Gaza bila ya kujali madhara yake, na katika hali hii haiwezekani kuendelea shughuli za baraza la mawaziri. Huku hali ya Tel Aviv ikizidi kuwa mbaya, kuna uwezekkano wa kutokea anguko la kisiasa na Netanyahu atalazimika kuitisha uchaguzi wa mapema.