Hizbullah: Irada ya Walebanon, ndiyo silaha kubwa zaidi ya Muqawama
Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon imepongeza hatua ya kurejea maelfu kwa maelfu ya watu katika miji yao ambayo ingali inakaliwa kwa mabavu kusini mwa Lebanon, huku wakipuuzilia mbali vitisho vya jeshi la Israel, ikisema nia yao isiyo na kikomo na moyo wao usioweza kutetereshwa, ndiyo silaha kali zaidi za mrengo wa Muqawama.
Harakati ya Hizbullah imeieleza Januari 26 (jana Jumapili) kama "Siku Tukufu ya Allah" na "onyesho kubwa la heshima na izza lililobuniwa na Wanamuqawama.
Kwa mujibu wa mamlaka za Lebanon, wanajeshi wa Israel waliwauwa shahidi watu 22 kusini mwa nchi hiyo ya Kiarabu jana Jumapili, wakati muhula wa kuondoka kwa wanajeshi wa Kizayuni ulipomalizika, huku maelfu ya raia wa Lebanon wakijaribu kurejea makwao.
Hizbullah imepongeza uthabiti na kusimama kidete watu wa Lebanon, ikiashiria uhusiano wao wa karibu na nchi yao, kushikamana kwao barabara na kila shibri ya ardhi ya Lebanon, jukumu lao thabiti la kuwa walinzi wa mamlaka ya kujitawala taifa, na ustahimilivu wao usio na shaka dhidi ya vitisho na vitendo vyote vya uchokozi.
Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limekiuka makubaliano ya kusimamisha vita kwa kuwashambulia raia wa Lebanon ambao walikuwa njiani wakirejea majumbani kwao katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.
Wizara ya Afya ya Lebanon imeripoti kuwa, tangu jana asubuhi hadi sasa, makumi ya Walebanon wameuawa shahidi na wenegine zaidi ya 80 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni kusini mwa Lebanon.