UN: Zaidi ya Wanafunzi 100,000 Wamerejea Shuleni Ukanda wa Gaza
(last modified Sat, 01 Mar 2025 03:49:49 GMT )
Mar 01, 2025 03:49 UTC
  • UN: Zaidi ya Wanafunzi 100,000 Wamerejea Shuleni Ukanda wa Gaza

Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa zaidi ya wanafunzi 100,000 wamejiandikisha mashuleni katika Ukanda wa Gaza baada ya mwaka mpya wa masomo kuanza Februari 23, na kuashiria kurudi mashuleni wanafunzi baada ya muda mrefu wa kusimamishwa masomo kutokana na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kiziayuni wa Israel dhidi ya watu wa eneo hilo la Palestina.

Kufunguliwa shule huko Gaza ni hatua muhimu ya kurejesha elimu katika eneo hilo lililoathiriwa sana na vita. Japokuwa 85% ya shule hazifanyi kazi kutokana na mashambulizi ya Israel, kurudi madarasani wanafunzi wa Gaza ni kielelezo cha matumaini kwa familia nyingi na fursa kwa watoto kurejea katika hali ya kawaida.

Kufikia Februari 27, 2025, Umoja wa Mataifa ulithibitisha kuwa shule za umma 165 zimefunguliwa tena huko Gaza na kuruhusu wanafunzi kuanza tena masomo yao baada ya kusimama kwa miezi 16. Vita na mauaji ya kimbari ya Israel yaliyoanza Oktoba 2023 yamekuwa na athari mbaya na hasara kubwa kati ya wanafunzi, walimu na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya elimu.

Israel imeua wanafunzi wasiopungua 12,800 na walimu 800, huku taasisi 1,166 za elimu zikiharibiwa. Uharibifu wa mashambulizi ya Israel katika sekta ya elimu huko Gaza unakadiriwa kuwa wa zaidi ya dola bilioni 2.