UN: Wapalestina 400,000 Gaza wamefurushwa makwao ndani ya wiki 3
Takwimu mpya za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, idadi kubwa ya Wapalestina wamelazimika kuyahama makazi yao katika Ukanda wa Gaza tangu utawala haramu wa Israel uanzishe mashambulizi mapya baada ya kuvunja makubaliano ya usitishaji vita zaidi ya wiki tatu zilizopita.
"Inakadiriwa kuwa, karibu watu 400,000 wamekimbia makazi yao huko Gaza kufuatia kuvunjika kwa (makubaliano ya) usitishaji mapigano," Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) lilisema katika ujumbe uliotumwa kwenye mtandao wa kijamii wa X jana Ijumaa.
Zaidi ya watu milioni mbili wanaishi katika eneo hilo la pwani, ambalo liko chini ya mzingiro wa kibaguzi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Jeshi la Israel limekuwa likiwataka wakazi wa Gaza kuondoka katika makazi yao, kwa kisingizio kuwa linataka kufanya operresheni dhidi ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas.
Wakati huo huo, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wameendelea kushambulia makazi ya watu huko Gaza.
Hujuma ya karibuni kabisa wa Wazayuni imelenga nyumba moja huko Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza na kuua shahidi watu 10 wa familia moja, shirika la habari la Palestina WAFA liliripoti Ijumaa.
Mashambulizi mapya ya kinyama ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Gaza hadi sasa yameshawaua shahidi zaidi ya Wapalestina 1,500 tangu jeshi la utawala huo ghasibu livunje makubaliano ya usitishaji vita Machi 18.