Ayatullah Sistani: Papa Francis alikuwa na hadhi ya juu kiroho mbele ya mataifa mengi
Apr 22, 2025 08:47 UTC
Kiongozi Mkuu wa kidini wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq Ayatullah Sayyid Ali Sistani amesema, Papa Francis alikuwa na hadhi ya juu kiroho mbele ya mataifa mengi kutokana na mchango wake wa kipekee katika kuhimiza amani na kuvumiliana pamoja na kuonyesha mshikamano na watu wanaodhulumiwa duniani.
Ofisi ya Ayatullah Sistani, Marjaa Taqlidi wa Waislamu wa Kishia nchini Iraq, imetoa taarifa ya salamu za rambirambi kwa kufariki dunia Papa Francis, Kiongozi wa Wakatoliki duniani, na kueleza kwamba, Papa Francis alikuwa na hadhi ya juu kiroho mbele ya mataifa mengi na aliheshimiwa na watu wote kwa kuhimiza amani na kuvumiliana na kuonyesha mshikamano kwa watu wanaodhulumiwa na wanaokandamizwa duniani kote.
Taarifa ya ofisi ya Ayatullah Sistani imeendelea kueleza kwamba, mkutano wa kihistoria baina ya Papa Francis na Ayatullah Sistani ambao ulifanyika katika mji wa Najaful-Ashraf ulikuwa na umuhimu mkubwa kutokana na pande zote mbili kutilia mkazo nafasi kuu ya imani.

Ayatullah Sistani amesisitizia pia ulazima wa kufanyika juhudi za pamoja kwa ajili ya kuimarisha utamaduni wa kuishi pamoja kwa amani, kujiepusha na chuki na vitendo vya utumiaji nguvu, na kutilia mkazo thamani na tunu zinazokubaliwa na watu wote kwa msingi wa kuchunga haki na kuheshimiana wafuasi wa dini na mielekeo mbalimbali ya kifikra.
Vatican ilitangaza rasmi jana kwamba Papa Francis amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88.
Papa, ambaye alikuwa Askofu Mkuu wa Roma na Mkuu wa Kanisa Katoliki, alichukua wadhifa huo mwaka 2013 baada ya kujiuzulu mtangulizi wake, Benedict XVI.../
Tags