Tahadhari kuhusu maafa ya kibinadamu ya Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i1531-tahadhari_kuhusu_maafa_ya_kibinadamu_ya_yemen
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa mashambulizi yanayoendelea kufanywa na ndege za kivita za Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya watu wa Yemen yanaitumbukiza nchi hiyo katika maafa makubwa ya kibinadamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 19, 2016 04:25 UTC
  • Tahadhari kuhusu maafa ya kibinadamu ya Yemen

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa mashambulizi yanayoendelea kufanywa na ndege za kivita za Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya watu wa Yemen yanaitumbukiza nchi hiyo katika maafa makubwa ya kibinadamu.

Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Ismail Ould Sheikh Ahmad ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba uharibifu mkubwa wa vituo vya afya, huduma mbalimbali na maghala ya kuhifadhi chakula unaosababishwa na mashambulizi ya anga ya Saudi Arabia unaitumbukiza Yemen katika maafa makubwa ya kibinadamu. Sheikh Ahmad ametahadharisha kuhusu hali mbaya ya watu wa Yemen na kusema: Mapigano yameshadidi zaidi katika maeneo ya Aden, Shibu, Lahaj na katika mji mkuu, San'aa na kwamba mashambulizi yanayolenga vituo vya ukaguzi vya jeshi la Yemen, nyumba za makamanda wa jeshi na maafisa usalama yametayarisha uwanja wa kuwepo na kushamiri makundi ya kigaidi nchini humo.

Tahadhari hiyo ya mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen imetolewa wakati shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limekemea vikali takwa la Saudi Arabia la kuondoka wafanyakazi wote wa kimataifa wa jumuiya za misaada ya kibinadamu nchini Yemen na kusisitiza kuwa, serikali ya Riyadh inawajibika kuheshimu sheria za kimataifa zinazoitaka ilinde jumuiya na taasisi za misaada ya kibinadamu huko Yemen.

Wiki iliyopita Saudi Arabia iliuandikia barua Umoja wa Mataifa ikiitaka jumuiya hiyo kuwaondoa wafanyakazi wake wote wa kimataifa katika maeneo yanayodhibitiwa na jeshi na makundi ya wapiganaji wa Yemen. Hata hivyo Umoja wa Mataifa ulisema kuwa, takwa hilo linapingana na sheria za kimataifa na kusisitiza kuwa, wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wa umoja huo wataendelea kutekeleza majukumu yao nchini Yemen licha ya mashinikizo ya Riyadh.

Kuongezeka kwa mashambulizi ya Saudi Arabia dhidi ya watu wa Yemen na kuzidishwa mzingiro wa pande zote wa watawala wa kifalme wa Riyadh dhidi ya taifa hilo kunafanyika licha ya taasisi na shakhsia wa kimataifa akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon kusisitiza udharura wa kukomesha mashambulizi hayo na kutahadharisha juu ya taathira zake mbaya.

Maafisa wa Yemen wanasema kuwa, kutokana na mapambano ya kishujaa wa watu wa Yemen dhidi ya wavamizi wa Kisaudia na washirika wao, sasa wavamizi hao wameelekeza mashambulio yao kwenye miundombinu kama taasisi za maji, vituo vya umeme, afya na usafirishaji na kuharibu taasisi za elimu, misikiti na kadhalika. Pamoja na hayo Wayemen wameendelea kusimama imara na kupambana kishujaa dhidi ya wavamizi hao na kupata mafanikio makubwa.

Saudi Arabia ikisaidiwa na Marekani na nchi kadhaa za Kiarabu, tarehe 26 Machi mwaka jana ilianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Waislamu wa Yemen na takwimu za kuaminika zinasema maelfu ya raia wasio na hatia yoyote wameuawa hadi sasa katika mashambulizi hayo wengi wao wakiwa watoto wadogo, wanawake na wazee.