Magaidi wazidi kuangamizwa katika maeneo tofauti ya Syria
-
Wanajeshi wa Syria wakiwa katika operesheni za kukabiliana na magaidi wanaoungwa mkono na madola ya kibeberu
Habari kutoka nchini Syria zinasema kuwa, makumi ya magaidi wanaendelea kuuawa katika mashambulizi ya jeshi la Syria na ndege za Russia.
Televisheni ya al Alam imetangaza leo kuwa, mashambulizi ya ndege za Russia katika kambi ya al Sifr, mkoani Hama, kaskazini magharibi mwa Syria, yameua makamanda 50 wa makundi ya kigaidi pamoja na wanamgambo wengine kadhaa.
Aidha vyombo vya habari vya Syria vimetangaza habari ya kuangamizwa wakuu watatu wa magenge ya kigaidi katika mikoa miwili ya Dar'a na Halab, kusini na kaskazini mwa Syria. Magaidi hao ni wa kundi la Ahrar al Sham.
Vile vile wanajeshi wa Syria, jana walishambulia kwa maroketi magari kadhaa ya ya magaidi wa Ahrar al Sham magharibi mwa Halab. Magaidi wengi wa kundi hilo wanapatikana katika mikoa ya Idlib (kaskazini magharibi), Halab na Hama.
Wakati huo huo jeshi la Syria limetoa muda maalumu wa kuondoka magaidi katika mji wa Halab, kaskazini mwa nchi hiyo.
Shirika la habari la Associated Press limeinukuu komandi kuu ya jeshi la Syria ikiwataka magaidi wote walioko mashariki mwa mji wa Halab waondoke haraka kwenye eneo hilo, vinginevyo wajiandae kwa mashambulizi makali kutoka kwa jeshi la nchi hiyo.