Magaidi zaidi waangamizwa katika mkoa wa Salahuddin nchini Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i17623-magaidi_zaidi_waangamizwa_katika_mkoa_wa_salahuddin_nchini_iraq
Jeshi la Iraq limetangaza habari ya kushadidisha mashambulizi yake katika mkoa wa Salahuddin wa kaskazini mwa Baghdad, mji mkuu wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 17, 2016 12:23 UTC
  • Magaidi zaidi waangamizwa katika mkoa wa Salahuddin nchini Iraq

Jeshi la Iraq limetangaza habari ya kushadidisha mashambulizi yake katika mkoa wa Salahuddin wa kaskazini mwa Baghdad, mji mkuu wa nchi hiyo.

Televisheni ya al Sumariya News imeripoti kuwa, ndege za jeshi la Iraq, leo zimefanya mashambulizi makubwa dhidi ya maeneo ya magaidi wa ISIS katika mji wa al Shirqat, kaskazini mwa mkoa wa Salahuddin na kuangamiza kambi tano za genge hilo la kigaidi. Kwa mujibu wa habari hiyo, wanamgambo kadhaa wa Daesh wameuawa kwenye mashambulizi hayo.

Mashambulio hayo yamefanyika sambamba na kuanza operesheni ya kuikomboa Mosil kutoka mikononi mwa Daesh ambapo jeshi la Iraq kwa kushirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi maarufu kwa jina la al Hashdu al Shaabi, wamefanya mashambulizi makali dhidi ya maeneo ya mgaidi hao mjini Mosul. Huku hayo yakiripotiwa, habari nyingine zinasema kuwa, genge la Daesh limeua wapiganaji wake kadhaa kwa tuhuma za kujaribu kufanya mapinduzi dhidi ya Abubakar al Baghdadi, mkuu wa genge hilo la kigaidi.

Genge la kigaidi la Daesh lazidi kusambaratika

 

Wakati huo huo Spika wa Bunge la Iraq, Salim al Jabouri amevitaka vikosi vya serikali vifanye kadiri vinavyoweza kuhakikisha vinapunguza mno hasara za raia katika operesheni ya ukombozi wa Mosul.

Serikali ya Iraq imewataka raia na wananchi wa kawaida wabakie majumbani mwao. Hata hivyo wakuu wa genge la Daesh ambao wameifanya Mosul kuwa makao yao makuu, wamekata umeme na mawasiliano yote ili kuwazuia wakazi wa mji huo kupata habari kutoka nje ya Mosul.