Iraq: Nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi, wafadhili wa Daesh
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i17659-iraq_nchi_za_kiarabu_za_ghuba_ya_uajemi_wafadhili_wa_daesh
Waziri Mkuu wa Iraq amesema nchi kadhaa za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi zinaliunga mkono na kulifadhili kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, linalofanya jinai za kutisha nchini humo na Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 18, 2016 03:38 UTC
  • Iraq: Nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi, wafadhili wa Daesh

Waziri Mkuu wa Iraq amesema nchi kadhaa za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi zinaliunga mkono na kulifadhili kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, linalofanya jinai za kutisha nchini humo na Syria.

Haider al-Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq ameyasema hayo katika mkutano wake na mabalozi wa nchi za kigeni na kuongeza kuwa, Saudi Arabia ndiyo kinara wa nchi za Kiarabu zinazounga mkono harakati za kundi hilo la wakufurishaji.

Waziri Mkuu wa Iraq amesema haiwekezani kuwa kundi la kigaidi la Daesh lilichipuka tu usiku mmoja akisisitiza kuwa, magaidi hao wamekuwa wakipokea msaada wa kifedha na silaha kutoka nchi fulani za Kiarabu katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Jeshi la Iraq likielekea mji wa Mosul, Iraq

Ameongeza kuwa, ufadhili huo huo ndio uliolisaidia kundi la kigaidi la Daesh/ISIS kuuteka mji wa Mosul, kaskazini mwa nchi, mji ambao kwa sasa unashuhudia mashambulizi makali ya jeshi la Iraq linalopania kuukomboa kikamilifu. mji huo unahesabiwa kuwa ngome ya mwisho ya genge la Daesh.

Hii ni katika hali ambayo, Jeshi la Iraq limetangaza habari ya kushadidisha mashambulizi yake katika mkoa wa Salahuddin kaskazini mwa Baghdad, mji mkuu wa nchi hiyo.

Kwa muda mrefu mji wa Mosul umekuwa ngome kuu ya Daesh

Ndege za jeshi la Iraq, jana Jumatau zilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya maeneo ya magaidi wa ISIS katika mji wa al Shirqat, kaskazini mwa mkoa wa Salahuddin na kusambaratisha kambi tano za genge hilo la kigaidi. Kwa mujibu wa habari hiyo, wanamgambo kadhaa wa Daesh wameuawa kwenye mashambulizi hayo.