Kaburi la umati lagunduliwa karibu na Mosul nchini Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i19039-kaburi_la_umati_lagunduliwa_karibu_na_mosul_nchini_iraq
Vikosi vya serikali ya Iraq vimegundua kaburi la umati karibu na mji wa Mosul ambao kwa sasa unashuhudia makabiliano makali kati ya vikosi hivyo na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh/ISIS.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 08, 2016 04:15 UTC
  • Kaburi la umati lagunduliwa karibu na Mosul nchini Iraq

Vikosi vya serikali ya Iraq vimegundua kaburi la umati karibu na mji wa Mosul ambao kwa sasa unashuhudia makabiliano makali kati ya vikosi hivyo na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh/ISIS.

Brigedia Jenerali Yahya Rasool, msemaji wa Komandi ya Pamoja ya Vikosi vya Iraq amesema kuwa, kaburi hilo la umati limepatikana likiwa na miili 100 katika mji wa Hammam al-Alil, yapata kilomita 14 kusini mwa Mosul.

Ameongeza kuwa, miili hiyo inaashiria kuwa watu hao waliteswa na kukatwa viungo vyao vya mwili kama mikono na miguu kabla ya kuuawa. Hata hivyo amebainisha kuwa, uchunguzi wa kimaabara wa kuitambua miili hiyo utafanyika leo Jumanne.

Mapambano ya kuitokomeza Daesh mjini Mosul, Iraq

Kwa upande wake Brigedia Jenerali Ali al-Lami, kamanda mkuu wa jeshi la Iraq amesisitiza kuwa, miili hiyo ni ya raia waliouawa na wanamgambo wa kitakfiri wa Daesh baada ya kukataa kuunga mkono harakati za magaidi hao.

Mapema jana, wanajeshi wa Iraq waliingia katika eneo la kwanza kabisa la makazi ya watu kaskazini mwa Mosul baada ya kuwashinda nguvu wanamgambo wa genge la kigaidi la Daesh na kufanikiwa kukomboa kijiji cha al Raziqiyyah kutoka mikononi mwa kundi hilo la kitakfiri.

Hadi sasa jeshi la Iraq kwa kushirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi limefanikiwa kukomboa vijiji na maeneo 180 ya mkoa wa Nainawa tangu ilipoanza operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul kaskazini mwa Iraq tarehe 17 mwezi uliopita wa Oktoba.