Jaafari: Thuluthi moja ya Mosul imekombolewa na vikosi vya Iraq
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesema jeshi la nchi hiyo likishirikiana na vikosi vya kujitolea vya wananchi vimefanikiwa kukomboa thuluthi moja ya mji wa Mosul toka mikononi mwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.
Ibrahim al-Jaafari aliyasema hayo jana Jumatatu katika mkutano wake na Frank-Walter Steinmeier, Waziri wa Mambo ya Nje ya Ujerumani mjini Berlin na kuongeza kuwa, operesheni ya kuukomboa mji huo inaendelea kupata mafanikio makubwa na kwamba hadi sasa wameangamiza magaidi 1000 na kukamata wengine 650.
Kadhalika amesisitiza kuwa, serikali ya Iraq haitaruhusu wala kufumbia macho ungiliaji wowote wa vikosi vya Uturuki katika mipaka ya nchi mbili hizo, siku chache baada ya duru za kiusalama za Ankara kuripoti kuwa, tayari Uturuki imetuma vifaru 30 na zana za kivita katika mji wa Silopi, kusini mashariki mwa eneo la mpaka wa nchi mbili hizo.
Hii ni katika hali ambayo, ofisa wa ngazi za juu katika Polisi ya Iraq, Jenerali Shaker Jodat amesema wanajeshi wamechukua udhibiti wa eneo lenye ukubwa wa kilomita mraba 1,850 kusini mwa Mosul kutoka mikononi mwa magaidi wa ISIS au Daesh sambamba na kuziokoa familia zaidi ya 10,000 zilizokuwa zikishikiliwa mateka hapo.
Operesheni ya kukomboa Mosul ambayo ni makao makuu ya mkoa wa Nainawa (Nineve) nchini Iraq ilianza tarehe 17 mwezi uliopita wa Oktoba ambapo magaidi wa Daesh wanaendelea kufurushwa kutoka maeneo mengi ya mji huo.