Ripoti: Genge la Daesh linawashikilia Mayazidi 3500 wa Iraq
Kiongozi wa ofisi ya kufuatilia masuala ya raia wa Iraq wa kabila la Yazidi amesema kuwa, hadi sasa wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh wanawashikilia mateka watu wa kabila hilo wapatao 3500.
Hussein Qaidi, ameyasema hayo katika kikao na waandishi wa habari mjini Dahuk, kaskazini mwa Iraq na kuongeza kuwa, jeshi la Iraq linaendeleza juhudi za kuwakomboa Wairaq hao wa kabila la Yazidi wakiwemo wanawake na wanaume. Amefafanua kuwa, tangu mwezi Agosti mwaka 2014, jumla ya Mayazidi 2000 na 782 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto waliokuwa wakishikiliwa mateka na wakufurishaji hao, wameachiliwa huru.
Tarehe 16 Juni mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, kundi la kigaidi la Daesh limefanya jinai kubwa ya mauaji ya umati dhidi ya Mayazidi wa Iraq na kwamba kundi hilo linakusudia kuangamiza kabisa watu wa kabila hilo. Baada ya kukaliwa kwa mabavu mji wa Sinjar ulio katika mkoa wa Nineve (Nainawa) na Mosul huko kaskazini mwa Iraq mwaka 2014, kundi la Daesh (ISIS) liliwateka nyara maelfu ya watu wa kabila la Yazidi wa miji hiyo. Mji huo wa Sinjar ulikaliwa kwa mabavu tarehe tatu Agosti mwaka 2014, baada ya kurudi nyuma wapiganaji wa Kikurdi wa Peshmerga.
Hata hivyo tarehe 13 Novemba mwaka jana, wapiganaji wa Peshmerga kwa kushirikiana na wanamgambo wa kiraia tawi la harakati ya PKK, walifanikiwa kuukomboa mji huo wa Sinjar kutoka mikononi mwa magaidi hao wa Daesh.
Operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul ilianza tarehe 17 Oktoba mwaka huu kwa amri ya Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi. Operesheni hiyo unafanyika kwa mafanikio makubwa, nasehemu kubwa ya mji huo tayari yamekombolewa.