Misri yasisitiza kupambana na makundi ya kigaidi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i20536-misri_yasisitiza_kupambana_na_makundi_ya_kigaidi
Mwakilishi wa Misri katika Umoja wa Mataifa ametaka kuendeshwa mapambano na nchi zote dhidi ya makundi ya kigaidi.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Dec 01, 2016 04:07 UTC
  • Misri yasisitiza kupambana na makundi ya kigaidi

Mwakilishi wa Misri katika Umoja wa Mataifa ametaka kuendeshwa mapambano na nchi zote dhidi ya makundi ya kigaidi.

Balozi Amr Abul Atta Mwakilishi wa Kudumu wa Misri katika Umoja wa Mataifa alisema jana katika kikao cha Baraza la Usalama la umoja huo kilichoitishwa kuchunguza hali ya mambo ya mji wa Aleppo huko kaskazini mwa Syria kwamba, nchi zote zinapasa waziwazi kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa nchi hiyo.

Raia wa Syria wakiwa katika hali ngumu vitani huko Aleppo 

Balozi Amr Abul Atta amekosoa utendaji wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kushughulikia mgogoro wa Syria na kuongeza kuwa chombo hicho hadi sasa kimeshindwa kupata njia ya kuitoa Syria katika hali iliyonayo sasa. Mwakilishi wa Kudumu wa Misri katika Umoja wa Mataifa ameendelea kueleza kuwa, Cairo pamoja na washirika wake yaani Uhispania na New Zealand zinafanya jitihada ili kupatikana muafaka kwa uchache kuhusiana na kadhia ya Syria  khususan kuhusu mji wa Aleppo ; na kwa njia hiyo kupunguza matatizo ya kibinadamu nchini humo. 

Moja ya sehemu za mji wa Aleppo kama inavyoonekana baada ya mashambulizi

Jeshi la Syria siku kadhaa za hivi karibuni limefanikiwa kuwafurusha katika maeneo ya mashariki mwa Aleppo magaidi na wanamgambo wenye silaha wanaoungwa mkono na nchi za Magharibi. Duru zenye mfungamano na wanamgambo wenye silaha na magaidi mashariki mwa mji wa Aleppo zimearifu kuwa makundi hayo yanataka kufanya mazungumzo na serikali ya Syria na kuondoka katika mji huo.