Misri yaituhumu televisheni ya al Jazeera ya Qatar kuwa inaeneza fitna
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i22153-misri_yaituhumu_televisheni_ya_al_jazeera_ya_qatar_kuwa_inaeneza_fitna
Serikali ya Misri imesema kuwa, mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha al Jazeera cha Qatar ametiwa mbaroni kutokana na kueneza fitna.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 26, 2016 03:42 UTC
  • Misri yaituhumu televisheni ya al Jazeera ya Qatar kuwa inaeneza fitna

Serikali ya Misri imesema kuwa, mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha al Jazeera cha Qatar ametiwa mbaroni kutokana na kueneza fitna.

Mtandao wa habari wa an Nashra umeripoti habari hiyo kwa kunukuu taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri ikisema kuwa, Mahmoud Hussein Juma, mwandishi wa kituo cha televisheni cha al Jazeera cha Qatar ametiwa mbaroni kwa kueneza fitna na kufanya uchochozi dhidi ya taasisi za serikali kwa lengo la kuzusha fujo na machafuko nchini Misri.

Wakati huo huo Mwendesha Mashtaka Mkuu wa masuala ya usalama wa Misri amesema, sababu ya kutiwa mbaroni mwandishi huyo wa televisheni ya al Jazeera ya Qatar ni kueneza habari za uongo na uvumi usio na ukweli kuhusu hali ilivyo ndani ya Misri.

Maandamano nchini Misri

 

Itakumbukwa kuwa kituo cha televisheni cha al Jazeera cha Qatar kinatuhumiwa kueneza habari za uongo kuhusu matukio ya nchi nyinginezo kama vile Iraq na Syria na kushindwa kuficha hisia zake za kuyaunga mkono magenge yanayofanya mauaji na ukatili katika nchi hizo za Kiarabu.

Televisheni ya al Jazeera pia ina historia ya kuwa mstari wa mbele kuchochea watu kuandamana na kusimama dhidi ya tawala za nchi zao katika nchi kadha za Kiarabu, kama vile Libya, Tunisia na Misri na imekuwa ikilalamikiwa vikali kwamba inashughulikia habari za nchi nyingine na kuziacha za ndani ya Qatar ambayo watawala wake wanashirikiana kwa karibu na madola ya kibeberu hususan Marekani.