Jan 04, 2017 03:57 UTC
  • Al-Wefaq: Jamii ya kimataifa imefumbia macho mzingiro wa Diraz, Bahrain

Chama kikuu cha upinzani nchini Bahrain kimekosoa kimya cha jamii ya kimataifa juu ya mzingiro dhidi ya eneo la Diraz na ukandamizaji wanaofanyiwa wakazi wa eneo hilo kwa zaidi ya nusu mwaka sasa.

Sheikh Hussein al-Daihi, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho kikuu cha Waislamu nchini Bahrain ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: "Katika hali ambayo jamii ya kimataifa imekuwa ikilaani na hata kutoa mashinikizo ya kuvunjwa mizingiro ya kidhalimu katika maeneo mbali mbali ya dunia, lakini imeamua kufumbia macho kwa makusudi mzingiro katika eneo la Diraz."

Ameongeza kuwa, ni jambo la kusikitisha kwamba hakuna chombo chochote cha kimataifa kilichoamua kutuma japo jopo la kuchunguza mzingiro huo ambao umedumu kwa kipindi cha miezi sita sasa. Amefafanua kuwa: "Mzingiro huu wa zaidi ya siku 200 umewaathiri wakazi zaidi ya 20,000, hii ikiwa ni adhabu ya muda mrefu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya eneo hilo."

Maafisa usalama wakitumia mabomu ya kutoa machozi kuzima maandamano ya amani eneo la Diraz

Shaikh al-Daihi amebainisha kuwa, wakazi wa eneo la Diraz wanashuhudia kila aina ya dhulma na ukandamizaji kutoka maafisa usalama wa Bahrain huku akiitaka jamii ya kimataifa kukomesha misimamo yake ya kindumakuwili na kushughulikia kadhia ya Diraz.

Naibu Katibu Mkuu wa chama cha al-Wefaq ameongeza kuwa: "Licha ya mzingiro huo wa siku zaidi ya 200, lakini utawala wa Aal-Khalifa umeshindwa kuwanyamazisha wafuasi kindakindaki wa Sheikh Isa Qassim."

Wananchi wa Bahrain wamekuwa wakifanya maandamano ya kupinga kuvuliwa uraia Sheikh Isa Qassim kwa tuhuma zisizo na msingi kuwa eti anachochea malumbano ya kimadhehebu na ghasia. Sheikh Qassim ni mashuhuri kwa misimamo yake ya kutetea Umoja wa Kiislamu na maandamano ya amani Bahrain.

Maandamano ya Wabahrain kumuunga mkono Sheikh Qassim

 

 

Tags