Magaidi 250 wa Daesh waangamizwa mashariki mwa mji wa Mosul Iraq
Kamanda wa vikosi vya radiamali ya haraka vya Iraq jana usiku alitangaza habari ya kuangamziwa magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh wasiopungua 250 katika muda wa masaa 24 yaliyopita. Magaidi hao waliuawa katika oparesheni ya kuyakomboa maeneo ya mashariki mwa mji wa Mosul.
Tamer Mohammed Ismail kamanda wa vikosi vya radiamali ya haraka vya Iraq ameongeza kuwa vikosi hivyo vimewasababishia hasara kubwa magaidi wa Daesh huko mashariki mwa Mosul na kwamba maeneo mengi ya mashariki mwa mji huo yamekombolewa katika oparesheni hiyo. Kamanda Ismail amebainisha kuwa vikosi vyao pia vimefanikiwa kuzisambaratisha ndege tatu zisizo na rubani za Daesh ambazo zilikuwa na lengo la kuvishambulia vikosi vya Iraq. Kamanda wa vikosi vya radiamali ya haraka vya Iraq ameongeza kuwa katika kuendelea na oparesheni zake, vikosi hivyo tayari vimewasili katika eneo la al Intisar mashariki mwa mji wa Mosul na kuwaangamiza magaidi wote waliokuwepo katika eneo hilo.
Duru za Iraq awali zilitangaza pia habari ya kukombolewa eneo la al Wahda mashariki mwa mji wa Mosul. Vikosi vya Iraq aidha vimefanikiwa kuwaua magaidi wa Daesh waliokuwepo katika njia za kuelekea Mosul na Kirkuk. Oparesheni ya kijeshi ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka mikononi mwa kundi la Daesh, ambao ni makao makuu ya mkoa wa Nainawa huko kaskazini mwa Iraq ilianza tangu tarehe 17 mwezi Novemba mwaka jana kwa amri ya Waziri Mkuu Haidar al Abadi ambaye pia ni amiri jeshi mkuu wa majeshi ya nch hiyo. Maeneo mengi ya mji wa Mosul yamekombolewa na jeshi la Iraq tangu kuanza oparesheni hiyo hadi hivi sasa.