Mufti Mkuu wa Misri achaguliwa tena na jopo la maulamaa
Jopo la Maulamaa wa Misri kwa mara nyingine tena wamemchagua Shawki Abdulkareem Ibrahim Allam kuwa Mufti Mkuu wa nchi hiyo.
Jopo la Maulamaa wa Misri chini ya uongozi wa Ahmad Tayib Sheikhul Azhar limetangaza kuwa, duru ya uongozi wa Shawki Allam katika Darul Iftar ya Misri inamalizika tarehe Mosi mwezi Machi mwaka huu, hata hivyo jopo hilo limempigia kura nyingi mwanazuoni huyo likitaka aendelee kushikilia wadhifa huo kutokana na kuridhishwa na utendaji wake.
Wataalamu kwa upande wao wametoa maoni yao wakieleza kuwa, Shawki Allam amefanya kazi kubwa hususan kuhusu kupambana na fikra za kitakfiri na misimamo ya kuchupaji mipaka. Katiba ya Misri inasema kuwa, iwapo jopo la maulamaa wa nchi hiyo litambakisha wadhifani Mufti Mkuu wa nchi hiyo, basi Sheikh Mkuu wa al Azhar na Rais wa Misri pia wanapaswa kuafiki suala hilo.