Matokeo ya wakuu wa Misri kueneza chuki dhidi ya Ikhwanul Muslimin
Mahakama ya Misri imetangaza orodha mpya ya mamia ya watu ambao wametajwa kuwa wafuasi wa makundi ya kigaidi.
Kati ya walio katika orodha hiyo ya watuhumiwa wa ugaidi 1502 ni Mohammad Morsi, rais wa zamani aliyechaguliwa na wananchi na kisha kupinduliwa na jeshi, mchezaji maarufu wa soka aliyewahi kuchezea timu ya taifa ya Misri na timu ya Al Ahli, Mohamed Aboutrika, pamoja na wanachama wengine wa ngazi za juu wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin.
Majina mengine yaliyo katika orodha hiyo ya magaidi ya Misri ni kiongozi wa zamani wa Harakati ya Ikhwanul Muslimin Mehdi Akef, na naibu wake Kheirat Shater, jaji Walid Sharabi, na Mohammad Al Balataji ambaye ni miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu wa Ikhwanul Muslimin. Wengine walio katika orodha hiyo ya magaidi wa Misri ni pamoja na Abu A'ala Madhi mkuu wa chama cha upinzani cha Al Wasat, Bakinam al Sharqawi, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Misri.
Mahakama ya Misri pia imeiweka Haraakti ya Ikwanul Muslimin katika orodha ya makundi ya kigaidi nchini humo.
Serikali ya Misri inaisakama na kuikandamiza harakati ya Ikhwanul Muslimin katika hali ambayo hiyo ni moja ya taasizi za kale zaidi katika uga wa kisiasa na kidini nchini Misri na hivyo ina nafasi muhimu miongoni mwa jamii ya Wamisri. Hakuna shaka kuwa, kukandamiza na kupuuza harakati ya Ikhwanul Muslimin ni jambo ambalo litaandaa mazingira ya kuibuka ufa na mgawanyiko mkubwa katika jamii ya Wamisri.
Hali ya kisiasa ya Ikhwanul Muslimin ya Misri tokea mwaka 2011 inaweza kugawanywa katika sehemu mblili. Duru ya kwanza ni ya mwanzoni mwa mwaka 2012 hadi 2013. Katika kipindi hicho, Ikhwanul Muslimin ilifanikiwa kuingia madarakani na kuitawala Misri baada ya miaka 84 ya mapambano ya kisiasa nchini humo. Mbali na kupata ushindi katika uchaguzi wa bunge, Ikwanul Muslimin pia ilipata ushindi katika uchaguzi wa rais na mwanachama wake, Mohammad Morsi, akawa rais wa kwanza wa Misri kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia. Duru ya kunawiri kisiasa Ikhwanul Muslimin ilidumu kwa muda wa miezi 18 tu. Hivyo Ikhwan ilipambana kwa muda wa miaka 84 ili kufika madarakani lakini ilipopata ushindi haikuweza kulinda ushindi huo na ilitawala kwa miezi 18 tu.
Kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya Julai mwaka 2013, Mohammad Morsi aliondolewa madakarani na huo ukawa mwanzo wa kipindi kingine cha masaibu ya Ikhwanul Muslimin.
Hivyo kwa mara nyingine harakati hiyo ikawa upande wa upinzani wa serikali ya Misri ambayo iliitangaza Ikhwan kuwa harakati ya kigaidi. Hii ni katika hali ambayo Ikhanul Muslimin ni harakati yenye idadi kubwa zaidi ya wafuasi nchini Misri.
Tawala za kifalme za Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Kuwait zilifurahi na kupongeza hatua ya serikali ya Misri kutangaza Ikhwanul Muslimin kuwa kundi la kigaidi. Kwa kutumia kisingizio hicho cha kisheria kuwa Ikhanul Muslimin ni kundi la kigaidi, wakuu wa Misri walianzisha wimbi jipya la ukandamizaji dhidi ya wafuasi wa harakati hiyo ambapo wengi wamefikishwa mahakamani na hukumu za kidhalimu kutolewa dhidi yao.
Rais Abdel Fatah El Sisi wa Misri anasisistiza kuhusu kukandamizwa Ikhwanul Muslimin kwa visingizio kama vile kuhusika harakati hiyo na vitendo vya misimamo mikali ya kidini. Ukandamizaji huo utapalekea mgogoro kuibuka Misri na mgawanyiko katika jamii na hivyo kuifanya kazi ya El Sisi kuwa ngumu zaidi. Njia pekee ya Misri kujikwamua katika mgogoro uliopo ni kuwepo maelewano katika uga wa kisiasa nchini humo ili taifa hilo la Afrika Kaskazini liweze kustawi na kufikia malengo ya juu ya mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011 ambayo yalipelekea kuondoelwa madarakani diketeta Husni Mubarak ambaye aliitawala nchi hiyo kwa miongo mitatu.