Kuendelea ukandamizaji wa Israel dhidi ya mateka wa Kipalestina
Qadura Fares, Mkuu wa Klabu ya Mateka wa Kipalestina amesema kuwa, vitendo viovu wanavyofanyiwa Wapalestina hao kwa madai tofauti na kuongezeka sana jinai hizo dhidi ya mateka waKipalestina, ni mambo yanayofanyika kwa amri ya moja kwa moja ya Baraza la Mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mkuu huyo wa Klabu ya Mateka wa Kipalestina amesema, taasisi ya jela za utawala wa Kizayuni ndiyo inayopaswa kubeba dhima ya madhara yoyote wanayopata mateka wa Kipalestina.
Katika hali ambayo mateso na unyanyasaji wanaofanyiwa mateka wa Kipalestina na maafisa wa jela za Israel ukiwa umeongezeka sana hivi sasa, genge la utesaji la Israel limetumwa kwenye jela ya Nafha kwa ajili ya kuwatesa na kuwakandamiza vibaya zaidi mateka wa Kipalestina baada ya mateka wawili ambao walilikuwa wamechoshwa na unyanyasaji, kumjeruhi afisa mmoja wa Israel kwenye jela hiyo ya kuogofya. Hivi sasa wanajeshi wa Israel wanatumia kisingizio hicho kuongeza mateso dhidi ya mateka wa Kipalestina. Wanajeshi 400 wa Israel wameizingira jela ya Nafha na kuivamia kinyama na kikatili na baadaye kuwapiga na kuwatesa vibaya mateka wa Kipalestina kiasi kwamba, kwa mujibu wa Issa Qaraqe, mkuu wa timu ya kufuatilia masuala ya mateka wa Palesitna walioachiliwa huru, hali waliyo nayo mateka wa Kipalestina ni ya kutisha sana hivi sasa.
Kwa kweli madai yanayotolewa na wanajeshi katili wa Israel kujaribu kuhalalisha ukandamizaji na unyanyasaji wao mkubwa dhidi ya mateka wa Kipalestina ni madai ya kitoto kabisa ambayo kamwe hayastahiki kutumia nguvu zote hizo kukandamiza mateka wasio na ulinzi wowote. Hata hivyo unyanyasaji wanaofanyiwa mateka wa Kipalestina na utawala wa Kizayuni wa Israel haukuanza leo na unafanyika kwa shabaha maalumu. Moja ya shabaha kuu za unyanyasaji na mateso hayo makubwa, ni kujaribu kuwavunja moyo Wapalestina na kuwafanya waachane na muqawama na misimamo yao isiyotetereka. Israel inafanya ukandamizaji huo wa kuchupa mipaka dhidi ya mateka wa Kipalestina ili kuwafikishia ujumbe wanamapambano wa Palestina kwamba wakiendelea na mapambano yao dhidi ya uvamizi wa Israel, basi watakumbwa na unyanyasaji mkubwa kutoka kwa utawala wa Kizayuni. Hata hivyo jambo ambalo utawala wa Kizayuni wa Israel unajaribu kujisahaulisha kwa hila hali ni uhakika kwamba, ukatili na ukandamizaji huo kamwe hauwezi kulizuia taifa la Palestina kusimama imara kupigania haki zake.
Sababu nyingine ya kimsingi inayoufanya utawala wa Kizayuni wa Israel ufanye ukatili na unyanyasaji mkubwa dhidi ya mateka wa Palestina na dhidi ya Wapalestina wote kiujumla, ni kutokana na kuwa na yakini viongozi wa Israel kwamba wanaweza kufanya ukatili wa aina yoyote ile bila ya kuguswa na madola ya Magharibi wala Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Vitendo vya madola ya Magharibi vinaonesha wazi kuwa, katika fikra zao, madola hayo yameuvua utawala wa Kizayuni na tuhuma zote kama jinai dhidi ya amani, jinai dhidi ya binadamu na jinai za kivita.
Jambo hilo limezidisha ujuba wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao hivi sasa unakataa hata kuwaachilia huru mateka wa Kipalestina ambao muda wa vifungo vyao umeisha. Bilal Kayed ni mmoja wa mateka hao ambao kifungo chake cha miaka 14 na miezi sita kimemalizika, lakini Israel inakataa kumwachilia huru. Si hayo tu, lakini pia kuna idadi kubwa ya Wapalestina wanaokufa shahidi katika jela za kutisha za Israel kutokana na mateso na kutopewa huduma zinazotakiwa za kiafya, lakini hakuna yoyote anayenyanyua sauti ya angalau kulaani tu ukandamizaji huo mkubwa wa Israel dhidi ya mateka wa Kipalestina; si madola ya Magharibi, wala Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na wala mashirika yanayojidai kutetea haki za binadamu duniani.