Palestina: Baraza la Usalama lifanye kikao haraka kujadili ujenzi wa vitongoji
Wizara ya Mambo ya Nje ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imetoa taarifa ya kutaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liitishe kikao cha haraka ili kuchukua hatua zinazotakiwa kuzuia ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni unaoendelea kufanywa na utawala haramu wa Israel na ukiukaji wa maazmio ya kimataifa unaofanywa na utawala huo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imetangaza leo kuwa inafuatilia kwa uzito kamili hatua na radiamali za kieneo na kimataifa kuhusiana na uamuzi wa bunge la utawala wa Kizayuni wa kupitisha sheria iitwayo "Sheria ya Mapatano" ya kuhalalisha ujenzi wa maelfu ya vitongoji katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imekosoa kimya ambacho hakikubaliki cha baadhi ya nchi, zikiongozwa na Marekani, na kueleza kwamba madamu kulaani kwa maneno ujenzi wa vitongoji hakufuatishwi na uchukuaji hatua za kivitendo za kuuadhibu utawala wa Kizayuni na wala hakuathiri chochote katika uhusiano wa pande mbili baina ya mataifa ya ulimwengu na Tel Aviv, utawala huo ghasibu utaendeleza ujenzi haramu wa vitongoji; na radiamali kauli za maneno matupu yanayotolewa dhidi yake yatazidi kuuhamasisha na kuushajiisha uendelee kukiuka waziwazi sheria za kimataifa kupitia upanuzi wa vitongoji hivyo.
Katika muendelezo wa ujenzi wa vitongoji katika ardhi za Wapalestina na kukiuka waziwazi azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kamati ya ujenzi wa vitongoji ya utawala wa Kizayuni wa Israel jana ilipitisha uamuzi wa kujengwa fleti nyingine mpya 181 katika mji wa Baitul Muqaddas…/