Mafanikio makubwa huko Iraq; kukimbia Daesh kutoka Mosul hadi Raqqa
Ushindi vilioupata vikosi vya jeshi la Iraq katika mji wa Mosul kukiwemo kudhibiti majengo muhimu ya serikali umewapelekea makamanda wa kundi la kigaidi la Daesh kuwataka magaidi waukimbie mji wa Mosul na kuelekea Raqqa nchini Syria.
Eneo la Magharibi mwa mji wa Mosul linakaribia kukombolewa kutoka mikononi mwa magaidi wa kundi la Daesh kufuatia ushindi viliopata vikosi vya Iraq siku mbili zilizopita. Majengo ya serikali na yale muhimu likiwemo jengo la gavana wa mji wa Nainawa, jumba la turathi za kale, majengo ya ofisi za mahakama, idara ya polisi na ile ya maji na umeme hivi sasa yamekombolewa kutoka mikononi mwa magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh. Haidar al Abadi Waziri Mkuu wa Iraq pia amewasili Mosul na kupongeza kukombolewa majengo ya serikali na ofisi ya gavana mjini humo na kuitaja hatua hiyo kuwa ni mafanikio makubwa katika oparesheni ya kijeshi iliyotekelezwa huko Mosul.
Mji wa Mosul unafahamika kama ngome muhimu na ya mwisho iliyokuwa ikishikiliwa na magaidi wa Daesh huko Iraq. Sehemu ya mashariki mwa Mosul ilikombolewa kikamilifu tarehe 24 mwezi Januari mwaka huu kutoka mikononi mwa magaidi wa kundi la Daesh. Oparesheni ya kulikomboa eneo la magharibi mwa mji wa Mosul ilianza tarehe 19 mwezi Februari mwaka huu. Sehemu ya eneo la magharibi mwa Mosul hivi sasa inakaribia kukombolewa na hadi kufikia sasa zimepita siku 17 pekee tangu kuanza oparesheni hiyo ya ukombozi. Matukio mbalimbali ya Mosul yanaonyesha kuwa kundi la kigaidi la Daesh limedhoofika zaidi nchini Iraq kuliko wakati mwingine wowote na sasa linakaribia kusambaratika. Moja ya dalili za kudhoofika kundi hilo huko Iraq ni namna oparesheni ya kuikomboa ofisi ya gavana wa Nainawa ilivyochukua muda wa masaa manne pekee. Wakati huo huo kama alivyotangaza Jenerali Abdulamir al Muhammadawi Msemaji wa kikosi cha radiamali ya haraka cha Iraq, kukombolewa majengo ya serikali huko al Dawsah Mosul kunamaanisha kufikia mwisho asilimia 80 ya oparesheni magharibi mwa mji huo.
Nukta yenye umuhimu ni hii kuwa magaidi wa Daesh pia wamekubali kupata pigo huko Mosul. Baada ya ushindi wa hivi karibuni wa vikosi vya Iraq katika mji huo, kundi la kigaidi la Daesh limewaamuru makamanda wake kuondoka mjini humo na kuelekea katika mji wa Raqqa. Jambo hilo linaonyesha mfungamano uliopo wa matukio yanayojiri huko Syria na Iraq. Katika siku za awali za kuanza oparesheni ya kuukomboa mji wa Mosul ilielezwa kuwa baadhi ya nchi za Kiarabu, za Magharibi pamoja na Uturuki ambazo zilikuwa zikiwaunga mkono magaidi mkabala na mafanikio vinayopata vikosi vya Iraq katika kuukomboa mji wa Mosul, zinafanya kila ziwezalo kuwahamisha magaidi hao kutoka Mosul na kuwapelekea katika maeneo tofauti ya Syria. Hata hivyo ushindi wa kistratejia wa jeshi la Syria na wanamuqawama katika kuukomboa mji wa Halab yaani Aleppo nchini humo umewashtua sana waungaji mkono hao wa magaidi.