WFP yaomba misaada ya haraka ya kibinadamu kwa ajili ya Yemen
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kwa mara nyingine tena limetahadharisha kuwa ukame na njaa vinatishia maisha ya raia karibu milioni 17 wa Yemen.
Mkurugenzi wa Shirika la WFP huko Yemen Stephen Anderson ameeleza kuwa, zinahitajika dola bilioni mbili na milioni mia moja ili kunusuru maisha ya mamilioni ya Wayemen wanaokabiliwa na ukosefu wa chakula.
Anderson ameashiria matatizo makubwa ya kifedha na vilevile ugumu unaolikabili shirika la WFP katika kuwafikia raia wanaohitaji misaada huko Yemen na kuongeza kuwa, Mpango wa Chakula Duniani hauna uwezo wa kuwahudumia raia wote wa Yemen wanaohitaji misaada.

Takwimu zinaonyesha kuwa, Wayemen zaidi ya milioni tatu wamekuwa wakimbizi, milioni 14 hawafikiwi na misaada ya kutosha ya chakula, na wengine milioni saba pia wanakaribia kuathiriwa na baa la njaa.
Saudia Arabia, ikiungwa mkono na Marekani na Uingereza, ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya raia wa Yemen tangu mwezi Machi mwaka juzi lengo likiwa ni kumrejesha madarakani kibaraka wao, Abdu Rabuh Mansour Hadi, Rais aliyejiuzulu wa Yemen na kukimbilia Riyadh. Raia zaidi ya elfu 11 wa Yemen wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa katika uvamizi huo wa kijeshi wa Saudia.