Mar 12, 2016 15:25 UTC
  • Amnesty: Huenda Saudia ikamnyonga mpwa wa Sheikh Nimr kesho!

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeelezea hofu yake kuwa yumkini utawala wa Saudi Arabia hapo kesho ukamnyonga Ali Nimr, mpwa wa Shahidi Sheikh Nimr Baqir al-Nimr, mwanachuoni mkuu na maarufu wa Kiislamu aliyenyongwa na watawala wa Aal-Saud mapema mwaka huu.

Amnesty International imeandika katika tovuti yake kuwa, familia ya Ali Nimr pamoja vijana wengine 2 wameelezea wasi wasi wao katika mitandao ya kijamii kuhusu uwezekano wa kutekelezwa hukumu ya kifo dhidi ya vijana hao hapo kesho. Ali Nimri pamoja na wenzake wawili Dawood Hussein al-Marhoon na Abdullah Hassan al-Zaher wanakabiliwa na tuhuma eti za ‘ugaidi’ kwa kushiriki maandamano ya kuikosoa serikali ya Riyadh. James Lynch, Naibu Mkurugenzi wa Amnesty International Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika amesema kuwa, iwapo hukumu hiyo itatekelezwa hapo kesho, basi utawala wa kifalme wa Saudia utadhihirisha namna usivyoheshimu sheria ya kimataifa, ambayo inapinga kuhukumiwa vijana kwa makosa waliyoyafanya kabla hawajatimiza miaka 18. Ali Nimr alikamatwa Februari mwaka 2012 wakati alikuwa na umri wa miaka 17, na kuhukumiwa kifo Mei mwaka 2014 mjini Jeddah, kwa mashtaka 12 likiwemo la kushiriki maandamano dhidi ya serikali. Itakumbukwa kuwa, Utawala wa Aal Saud tarehe Pili Januari mwaka huu ulimnyonga Sheikh Nimr Baqir al-Nimr, msomi mashuhuri wa Kishia, hatua iliyokabiliwa na wimbi kubwa la malalamiko kutoka nchi mbalimbali hususan katika ulimwengu wa Kiislamu.

Tags