Wapalestina 15 wameuawa shahidi tangu Wazayuni walipoanzisha chokochoko mpya Quds Tukufu
Duru za Palestina zimetangaza kuwa Wapalestina wasiopungua 15 wameuliwa shahidi tangu lilipoanza wimbi jipya la machafuko katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina hususan mji wa Baitul Muqaddas.
Wapalestina 15 wameuawa shahidi na wengine wapatao 1,400 wamejeruhiwa katika matukio ya karibuni ya msikiti wa Al-Aqsa na katika duru mpya ya mapigano kati ya waandamanaji wa Kipalestina na askari wa Kizayuni yaliyoanza tarehe 14 ya mwezi huu wa Julai huko Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan, Quds tukufu na Ukanda wa Gaza.
Wapalestina wawili waliuliwa shahidi na wengine 231 walijeruhiwa katika hujuma ya jana pekee Ijumaa iliyofanywa na askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
Machafuko katika Palestina inayokaliwa kwa mabavu yalishtadi kutokana na mapigano baina ya askari wa Kizayuni na Wapalestina kufuatia hatua ya utawala haramu wa Israel ya kufunga milango ya kuingilia msikiti wa Al-Aqsa.
Hatua ya kichochezi ya utawala wa Kizayuni ya kuifunga milango ya msikiti wa Al-Aqsa na kuweka mageti ya elektroniki iliamsha hasira za Waislamu.
Kabla ya hapo, viongozi wa Palestina walitaka jamii ya kimataifa iushinikize utawala wa Kizayuni ukomeshe vitendo vya ukatili na ukandamizaji dhidi ya Wapalestina na matukufu yao.../